Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali
imezitaka Halmashauri za Wilaya Nchini zinazopata mgawo wa mapato
yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu kutumia
asilimia 40 ya fedha hizo kwa ajili ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na
ulinzi wa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali
kama ilivyokubalika.
Hayo
yameelezwa jana Bungeni, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Japhet Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti
Maalum Mhe. Leah Jeremiah Komanya juu ya lini Serikali itaanza kupeleka
takwimu ya mapato yanayopatikana ili Halmashauri ziweze kujua stahiki
zake.
“Takwimu
za mapato yanayotokana na wanyamapori waliowindwa na upigaji picha
katika vitalu vya uwindaji na utalii wa picha nchini huandaliwa na
kutolewa taarifa mbalimbali,” alisema Mhe. Hasunga.
Aidha
amesema, Wizara imekuwa ikitoa mgawo wa asilimia 25 ya mapato
yatokanayo na ada ya wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu vilivyopo
kwenye maeneo ya wilaya husika.
Hata
hivyo amesema, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukalisha mfumo wa
kielektroniki ujulikanao kama “MNRT Portal” ambapo taarifa zinazohusu
Wizara ikiwa ni pamoja na mapato ya uwindaji wa kitalii zitapatikana
humo .
Mfumo
huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 01 Julai, 2018 ambapo nakala
ngumu za taarifa zitakuwa zikitumwa kwenda wilaya husika.
Wakati
huo huo Mhe. Hasunga alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum
Mhe. Maryam Salum Msabaha juu ya mkakati wa Serikali katika kuboresha
vivutio vya utalii nchini ikiwemo Bagamoyo ili kupata wageni wengi zaidi
na kukuza pato la Taifa, amesema Wizara imeandaa mkakati wa kuvitambua
na kuvitangaza vivutio vyote nchini ukiwemo mji wa Bagamoyo.
Amesema
mpango unalenga kushirikisha mashirika yaliyo chini ya Wizara yaani
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAMWA)
na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Ameendelea
kusema, vituo vya malikale vilivyopo Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo
yatakayoendelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika hayo. Aidha, vivutio
vyote vya utalii nchini vitaendelea kutangazwa kupitia Taasisi
zinazohusika ikiwemo Bodi ya utalii Tanzania (TTB).
Ametaja
kazi zitakazotekelezwa na mashirika hayo kuwa ni kuweka huduma muhimu
kwa watalii, kuboresha miundombinu ya vituo hususani majengo na barabara
ili kuwezesha kufikika kwa urahisi na kuwa na muonekano unaovutia ,
kujenga vituo vya kumbukumbu na taarifa pale ambapo vinahitajika,
kuboresha vioneshwa na kuvitangaza , kuhamasisha wawekezaji wa hoteli,
michezo na vivutio vingine vya watalii.
Hata
hivyo, Wizara ya MaliAsili na Utalii itaendelea kusimamia majukumu yote
ya uhifadhi, utafiti na kuandaa taarifazitakazosaidia kuboresha na
kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, kwa kutoa elimu kwa Umma
juu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya malikale na maliasili za nchi
yetu.
0 comments:
Post a Comment