Mbunge
wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amemsifu Rais John
Magufuli kwa kupeleka fedha za maendeleo katika halmashauri yake bila ya
kubagua, lakini amesema video iliyosambaa mitandaoni haitoi picha
halisi ya alichosema.
Video
hiyo fupi inamuonyesha Mchungaji Msigwa akizungumza kwenye hafla ya
chakula cha jioni iliyofanyika Ikulu ya Iringa juzi na kuhudhuriwa na
viongozi wa Serikali, wa kisiasa na kidini.
“Na
Mheshimiwa Rais umekuwa ukisisitiza kwenye hotuba zako kwamba wewe
hujali vyama na hili limedhihirika kwa kweli kwamba hujali vyama,”
anasema Mchungaji Msigwa katika video hiyo huku waalikwa wakimpigia
makofi.
“Umesaidia
sana. Bahati mbaya hawakukupangia ratiba ya kufungua miradi. Hela za
kutoka kwako zimekuja nyingi. Amezungumza Mheshimiwa (Waziri wa Mambo ya
Nje, Augustine) Mahiga, tuna barabara nzuri.
“Katika
kipindi chako ambacho umekuwa Rais tumejenga barabara ya lami ya mradi
wa World Bank kutoka Mlandege mpaka kwa mkuu wa wilaya, karibu Sh3.5
bilioni, tuna stendi nzuri iko hapo chini Ipogolo, karibu Sh3 bilioni.
Tuna maji. Kwa hiyo kuna vitu vimefanyika.
“Kwa
kweli Mheshimiwa Rais hupendelei, hata sisi wa Chadema unaleta hela.
Kwa hiyo wewe hujali vyama. Unaleta hela. Kwa hiyo wewe huwa hujali
vyama hilo nikupongeze sana.”
Wakati akisema hayo, picha zinaonyesha waalikwa wakiangua vicheko na sauti zao zinasikika wakati akihitimisha hotuba yake.
Msigwa
ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Serikali ya Awamu ya Tano na
alipotafutwa kuelezea kwa kirefu alichokizungumza alisema, “Wamechukua
kipande kidogo ambacho nilisema hela zimeletwa Manispaa ya Iringa,
lakini wameacha kipande kikubwa ambacho nilizungumza kwamba hata kama
madiwani wameondoka, Manispaa ya Iringa imekuwa nzuri, imekuwa bora,”
alisema jana.
“(Wanachama
wa Chadema na Ukawa) Wasione kama kuna mtu hapa ameyumba au nimesalimu
amri. Mapambano bado yanaendelea, hiyo ndiyo hoja.”
Kuhusu
alichokizungumza, alisema kauli yake ilimaanisha kuwa Manispaa ya
Iringa imekuwa bora katika kipindi hiki ambacho imekuwa chini ya Chadema
kwa kuwa Rais amekuwa akipeleka fedha bila ya kujali vyama, lakini
akashangaa kwamba ratiba yake mkoani Iringa haikujumuisha kutembelea
miradi mikubwa kama barabara, machinjio kubwa kuliko zote Tanzania,
stendi na mambo mengine.
“Kuna
miradi mingi imefanyika chini ya uongozi wetu ambayo haihusiani na
uwepo wa CCM ambao wapo katika manispaa hii na kumekuwa na dhana kuwa
watu wakiwa Chadema au kiongozi akiwa Chadema, hakuna maendeleo na ndio
maana madiwani wamekuwa wakihama,” alisema.
“Kwa
mfano, tuna barabara ambayo imejengwa kwa Sh3.5 bilioni na ambayo
haikuwapo. Tumejenga katika kipindi hiki ambacho manispaa inaongozwa na
Chadema.”
Pia
alisema kuna machinjio ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika mikoa ya
Nyanda za Juu Kusini, pamoja na stendi ya mabasi iliyokamilika.
0 comments:
Post a Comment