Ubunge
wa Maulid Mtulia wa Kinondoni (CCM), umewekwa rehani na aliyekuwa
mpinzani wake, Salum Mwalimu (Chadema) aliyefungua kesi akipinga matokeo
ya uchaguzi mdogo uliofanyika Februari 17.
Mtulia
aliibuka mshindi kwa kura 30,313 dhidi ya 12,353 alizopata Mwalimu.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Mtulia kujivua ubunge wa jimbo hilo
akiwa CUF na kujiunga na CCM iliyompitisha kugombea.
Mwalimu
amefungua kesi dhidi ya Mtulia; msimamizi wa uchaguzi ambaye ni
mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG).
Mbali
ya kesi ya msingi namba 129 ya mwaka 2018, Mwalimu amefungua maombi ya
kusamehewa au kupunguziwa kiwango cha fedha anachopaswa kukiwasilisha
mahakamani kama dhamana kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi hiyo.
Katika
kesi ya msingi, Mwalimu anaiomba mahakama itengue matokeo na itamke
kuwa uchaguzi ulikuwa batili, pamoja na mambo mengine akidai uligubikwa
na kasoro nyingi na mwenendo mbaya.
Anadai Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson wakati wa kampeni alitoa kauli za ubaguzi.
Katika
hati ya madai , Mwalimu anadai msimamizi wa uchaguzi alishindwa kutoa
fomu (kiapo cha siri) kwa mawakala wake wa vituo vya kupigia kura siku
saba kabla ya uchaguzi kinyume cha Kanuni za Uchaguzi za mwaka 2015.
Anadai
bila sababu za msingi, msimamizi wa uchaguzi alikataa na alishindwa
kuteua mawakala mbadala wa vituo vya kupigia kura licha ya kuwasilisha
kwake majina ya mawakala hao yaliyopendekezwa.
Pia,
anadai aliweka masharti mengine kwa mawakala wa vituo vya kupigia kura
akiwataka kuwa na kadi za utambulisho na barua za utambulisho kutoka kwa
msimamizi wa uchaguzi, aliloliweka siku ya upigaji kura.
Anadai
msimamizi alishindwa kuhakikisha usalama wa masanduku ya kupigia kura,
hivyo kusababisha moja katika kituo cha kupigia kura namba 3 kwenye Mtaa
wa Idrisa, Kata ya Magomeni kuhamishwa na watu wasiojulikana wakati wa
upigaji kura na kurejeshwa nusu saa baadaye.
Mwalimu
anadai timu ya kampeni ya Mtulia iliyomhusisha Dk Tulia ilitoa maneno
ya ubaguzi na yaliyompa haki isiyo sawa mpinzani wake.
Anadai maneno yaliyotolewa na Dk Tulia ni “Mkimchagua Mtulia nitampanga kukaa karibu na waziri mkuu.”
Mwalimu anadai mtiririko wa kasoro, ukiukwaji wa sheria na utaratibu uliathiri matokeo ya uchaguzi na demokrasia.
Mwanasiasa
huyo anaiomba mahakama ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mtulia
akidai uchaguzi haukuwa huru na wa haki, hivyo ni batili.
Katika
kesi za uchaguzi kila anayefungua kupinga matokeo anapaswa kuwasilisha
mahakamani Sh5 milioni kama dhamana ya usikilizwaji wa kesi kwa kila
mdaiwa. Kwa kawaida kesi za uchaguzi wadaiwa wa msingi huwa watatu;
mbunge aliyeshinda, msimamizi wa uchaguzi aliyemtangaza mshindi na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kama ilivyo kwa Mwalimu, anapaswa
kuwasilisha mahakamani Sh15 milioni kama dhamana ya usikilizwaji wa
kesi.
Hata
hivyo, Sheria ya Uchaguzi inatoa nafasi kwa mtu ambaye anadhani hana
uwezo wa kupata kiasi hicho cha fedha kuwasilisha maombi akiomba
kusamehewa zote au kupunguziwa kiwango. Kama mahakama itajiridhisha kuwa
hana uwezo basi inaweza kumsamehe au kumpunguzia kiwango na kumpangia
itakachoona inafaa.
Mwalimu
amewasilisha maombi mahakamani akiomba asamehewe kabisa au impunguzie
akidai si mbunge, hivyo hana uwezo wa kuweka kiasi hicho cha fedha.
Mashauri
hayo (kesi ya msingi pamoja na maombi), yaliyopangwa kusikilizwa na
Jaji Ignas Kitusi yalitajwa mahakamani jana. Jaji Kitusi ameelekeza
Mtulia apewe nyaraka za mashauri hayo baada ya kubaini hajapewa.
Mwalimu
aliwakilishwa na wakili Alex Masaba, huku msimamizi wa uchaguzi na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali,
Benson Hoseah. Mashauri hayo yaliahirishwa hadi Mei 14 yatakapotajwa.
0 comments:
Post a Comment