Mwanasheria
wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Gwakisa Mlawa, amedai
mahakamani kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo haikujua chochote
kuhusu mkataba ulioingiwa kati ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Tido Mhando
na Channel 2 Group Corporation (BV1).
Mlawa
alidai pia mshtakiwa anayekabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya
madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 887.1, aliingia
mkataba huo bila baraka za bodi ya zabuni ya TBC.
Shahidi huyo wa pili alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.
Akiongozwa
na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, shahidi huyo alidai
kuwa hakuwahi kuufahamu mkataba huo hadi alipopokea taarifa za kesi
Juni, 2012 kutoka Channel 2 Group Corporation (BV1) kwamba TBC imekiuka
mkataba wa kuwekeza mitambo ya digitali.
"Mheshimiwa
hakimu mkataba huo ulisainiwa kati ya Tido na watu wawili wa Channel 2
Group Corporation (BV1). Pia kulikuwapo na nyongeza ya mkataba uliotiwa
saini kati ya Juni, Agosti na Novemba mwaka 2008... TBC tulimwandikia
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuomba ushauri naye aliagiza ateuliwe
mwanasheria wa kimataifa ambaye ni mjuzi katika masuala hayo," alidai
shahidi na kuongeza kuwa:
"Iliteuliwa
kampuni ya uwakili ya Freshfield Bruckhaus Derringer us LLP ilikuja
nchini TBC kufanya uchunguzi wa nyaraka na kwamba ililipwa malipo ya
awali zaidi ya Sh. milioni 800...katika uchunguzi huo, ulibaini kuwa
Tido alisababisha hasara ya fedha hiyo iliyokuwa kampuni ya uwakili,"
alidai Mlawa.
Alipohojiwa
na wakili wa utetezi, Ramadhan Maleta, kama aliiona mikataba hiyo,
shahidi alidai kuwa ilikuwa kama wameingia makubaliano ya awali ya
maandalizi ya mchakato wa kuelekea kwenye digitali.
Katika
kesi ya msingi, inadaiwa kuwa Juni 16, 2008, akiwa Dubai, Umoja wa
Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, kwa
makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kutia saini mkataba wa
kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na
channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni, kitu ambacho ni
kinyume na Sheria ya Ununuzi na kuinufaisha BVl.
Katika
shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20,
2008 alipotia saini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati
ya TBC na BVl.
Katika
shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai,
Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano
kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa
utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika
shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido
alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa makubaliano kwa
kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati
ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Katika
shtaka la mwisho, anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008
akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh. 887,122,219.19.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo ushahidi wa Jamhuri.
0 comments:
Post a Comment