Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini Marco Mtunga amewaonya wanunuzi wa Pamba
watakaonunua pamba nje ya mfumo wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS)
na kuwa endapo watabainika Pamba hiyo itataifishwa na Serikali.
Onyo
hilo limetolewa Mkoani Simiyu katika kikao baina ya Viongozi wa mkoa
huo, viongozi wa vyama vya ushirika vya Msingi (AMCOS), wanunuzi wa
Pamba na Naibu Mrajisi kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dodoma
Charles Malunde, lengo likiwa ni kukumbusha juu ya uadilifu katika
masuala ya ununuzi wa pamba, ikiwa ni maandalizi wa ununuzi pamba baada
ya msimu kufunguliwa.
Mtunga
amesema mwaka huu Serikali imefanya uamuzi kwamba pamba yote
itakayozalishwa hapa nchini itanunuliwa kupitia Vyama vya Msingi (AMCOS)
jambo ambalo amesema limeelezwa vizuri katika mwongozo wa bodi.
“Tunawatahadharisha
wanunuzi wa pamba kufuata mfumo wa ununuzi wa pamba uliowekwa na
Serikali, pamba yote itakayokamatwa ikiwa haikununuliwa kupitia Chama
cha Ushirika cha Msingi itataifishwa na Serikali, katika mwongozo
tulioutoa maelekezo hayo yapo na yako chini ya sheria Namba 2 ya pamba
ya mwaka 2001” alisema Mtunga.
Kwa
upande wake Naibu Mrajisi kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dodoma
Charles Malunde amewataka viongozi wa Vyama vya ushirika kuepuka aina
yoyote ya wizi na ubadhilifu wa kutumia udanganyifu wa kuwaibia wakulima
kwa kuziharibu mizania.
Aidha,
Malunde amesisitiza sheria na taratibu za Ushirika zizingatiwe katika
uendeshaji wa Vyama vya Ushirika vya Msingi, hivyo akawataka viongozi
wote waliochaguliwa kuongoza vyama hivyo ambao wana shutuma zozote,
watumishi wa Umma au Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa kuachia
mara moja nafasi hizo kwa kuwa hawana sifa kwa mujibu wa sheria.
Baadhi
ya viongozi wa AMCOS waliwasilisha masuala mbalimbali kama maombi yao
kwa Serikali kuhusiana na ununuzi wa pamba ikiwa ni pamoja na kuomba
vyama vya ushirika vya msingi vipya vilivyo katika hatua ya usajili
vikamilishiwe usajili ili viweze kuingia katika mfumo huu wa ununuzi wa
pamba.
Akihitimisha
kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema anatamani
kuona ushirika wenye mtazamo wa kujibu changamoto na mahitaji ya
wakulima wa pamba, huku akitoa angalizo kwa viongozi wa AMCOS
watakaofanya ubadhilifu wa fedha za Vyama vya Ushirika kuwa Serikali
mkoani humo itawachukulia hatua kali.
“Ushirika
wa Simiyu (is my own baby) ni mtoto wangu mwenyewe, ni kitu ambacho
nilitamani kuona kinatokea, Wanaushirika wakakaokosa uadilifu wajihesabu
kuwa wafungwa watarajiwa, nawaambia nitawafunga na sitanii nitawafunga”
alisisitiza Mtaka.
Katika
hatua nyingine amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi
kuaandaa eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Chama Kikuu cha Ushirika
Simiyu.
0 comments:
Post a Comment