Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, wazazi wa kata tatu wilayani hapa Mkoa wa
Mara, wamemtaka mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nyanungu, Otieno
Nicholaus kuchagua kuhama au kupoteza maisha.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa mkutano wa wazazi uliofanyika hivi karibuni shuleni hapo.
Wazazi hao walimtuhumu mwalimu huyo kwa kuwapiga watoto hadi kuwajeruhi wanapokataa kulima shambani kwake.
Mmoja
wa wazazi wa watoto wanaodaiwa kupigwa, Muniko Sibora alisema Mei 7
mwalimu huyo alimpiga mwanaye baada ya kuvaa yeboyebo kutokana na kuwa
na kidonda mguuni.
Pia, alisema aliwapiga watoto wa Mwita Nyasongo na Ngocho Matiku kwa kuwa hawakwenda na majembe kupalilia mahindi yake.
“Huyu mwalimu anachofanya siyo sahihi, anatakiwa ahame vinginevyo mambo yatamharibikia,” alisema.
Kaimu
ofisa elimu wilaya, Hawamu Tambwe alikiri kupata taarifa hizo na kwamba
amemtuma mratibu elimu kata kufuatilia undani wa suala hilo na kupata
taarifa ya maandishi.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyanungu, Turuka Magabeu alikiri kupokea malalamiko ya wazazi kuhusu mwalimu huyo kuwapiga watoto.
“Inaelezwa katika tukio la mwisho aliwapiga na kuwaumiza watoto watatu kiasi cha kupelekwa hospitali,” alisema Magabeu.
Naye
mjumbe wa kamati ya shule hiyo, Museti Mwikwabe alisema Aprili 30
aliitisha kikao cha kamati lakini wajumbe walikataa wakiwamo wazazi
wote.
“Mei
4 aliwapeleka shambani watoto wakati wa masomo na tukamweleza, akaja
juu na Mei 7 akaamua kuwapiga na kuwaumiza watoto huku akiwaambia waje
watueleze wazazi,” alisema.
Mwalimu Otieno hakuweza kupatikana shuleni hata simu yake ilikuwa haipatikani kwa kile kilichodaiwa kuwa anaishi kwa kujificha.
Akizungumza
suala hilo, diwani wa Kyambahi, Mtoni Manyaki alikiri kupata taarifa
hizo na ameitisha kikao cha kamati ya maendeleo kata Mei 21 ili
kulijadili.
Naye
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya, Juma Hamsini alisema
baada ya kupata taarifa ameagiza timu yake kuchukua hatua haraka na
tayari wamepiga marufuku kuwatumia wanafunzi kulimia walimu.
“Hivi
karibuni katika Shule ya Msingi Mlimani kulikuwa na kesi kama hiyo
niliandika barua ya kupiga marufuku, wanafunzi wanaweza kulima shamba la
shule tena si wakati wa masomo,”alisema.
Polisi wilayani hapa wanadai wanaendelea kumsaka mwalimu huyo kuhusiana na tuhuma zilizowasilishwa.
0 comments:
Post a Comment