Baada ya kimya cha muda mrefu, hatimaye aliyekuwa Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ameibuka na kukabidhi ofisi na
akatoa ratiba ya shughuli zake katika Jimbo lake la Misungwi ikiwamo
ibada ya shukrani.
Kitwanga
ambaye uteuzi wake ulitenguliwa May 20 na Rais John Magufuli baada ya
kuingia bungeni na kujibu swali akiwa amelewa, alikabidhi ofisi jana kwa
Mwigulu Nchemba ambaye amechukua nafasi yake.
Baada ya uteuzi wake
kutenguliwa, Kitwanga alitoweka bungeni na baadaye ilielezwa kuwa
alikwenda Israel kabla ya hivi karibuni kurejea nchini na kusema kuwa
yote yaliyotokea anamwachia Mungu.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alimhamishia Mwigulu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutoka Wizara
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi huku Dk Charles Tizeba akimrithi Mwigulu.
Akizungumza katika mahojiano baada ya kukabidhi ofisi, Kitwanga alisema
kila Mtanzania anaweza kufanya kazi iwapo atapewa nafasi huku akinukuu
kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ na kwamba amefanya makabidhiano hayo kwa
wema na upendo wa hali ya juu.
Alisema amekabidhi ofisi bila kinyongo
kwa sababu Tanzania si nchi yake peke yake bali ni ya wananchi wote.
Ratiba jimboni
Akizungumzia ratiba jimboni mwake, Kitwanga alisema
Agosti 6, atafanya ibada ya shukrani nyumbani kwake Misungwi kumshukuru
Mungu akisema hiyo ni baada ya ziara yake ya wiki sita mfululizo kwa
wapigakura wake.
Ziara hiyo itaanza keshokutwa atakapokutana na kamati
ya mipango na fedha kabla ya kufanya kikao na madiwani wote wa jimbo
hilo Jumamosi ijayo.
Alisema Jumatatu ijayo atakabidhi vifaa mbalimbali
vikiwamo magodoro na vitanda kwa hospitali ya wilaya na zahanati,
vyerahani na kompresa kwa vikundi za ujasiriamali katika hafla
itakayofanyika kwenye Stendi ya Mabasi Misungwi: “Hapo nitatoa nafasi ya
dakika 10 mpaka 20 kwa waandishi wa habari kuniuliza maswali... lakini
nisingependa umbeya... kwangu mimi ni Tanzania kwanza, nawaambia kabisa.”
Baada ya shughuli hiyo, alisema siku inayofuata atakutana na wenyeviti
wa vijiji vyote vya jimbo hilo kupanga namna atakavyofanikisha ziara
yake katika maeneo yao, kazi ambayo alisema ataifanya kwa wiki sita
mfululizo; “nitafanya ziara siku tano kwa kila wiki mfululizo, zamani
nilikuwa nikigawa muda wa kutembelea jimbo na kurudi Dar kufanya kazi
sasa nitakuwa huko muda wote. Dar nitakuwa nakuja mara chache tu.”