GESI
ya helium ya takribani futi za ujazo bilioni 54 inayoelezwa kuwa adimu
duniani, imegundulika nchini Tanzania na kuiweka nchi kuwa miongoni mwa
mataifa machache yenye madini mengi na muhimu.
Wagunduzi
wa gesi hiyo ni watafiti kutoka vyuo vikuu viwili nchini Uingereza vya
Oxford na Durham kwa kushirikiana na wataalamu wa madini kutoka nchini
Norway.
Watafiti
hao wamegundua hifadhi kubwa zaidi duniani ya gesi hiyo ya barafu, kama
inavyofahamika katika eneo la Bonde la Ufa nchini.
Taarifa
za waandishi wa habari nchini Japan, zimeeleza kuwa watafiti hao
wamesema kuwa uhaba wa gesi hiyo duniani ulikuwa umesababisha taharuki
haswa kwa madaktari, ambao wanatumia gesi hiyo adimu kuendesha mashine
za utabibu zijulikanazo kama ‘MRI scanners’.
Pia hutumia katika mitambo ya kinyuklia na katika sekta nyingine nyingi za kiteknolojia.
Wiki
iliyopita, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati
akijibu swali bungeni mjini Dodoma alisema madini yanayotumika kwa
ajili ya mitambo ya Apollo na pia vifaa vya matibabu kama MRI na NMR,
yamegundulika kuwepo nchini Tanzania.
Hata
hivyo, hakufafanua zaidi kiasi cha madini hayo na namna nchi
itakavyonufaika na ugunduzi huo. Hata alipotafutwa jana, simu yake ya
mkononi ilipokewa na msaidizi wake na kueleza kuwa waziri yuko kikaoni.
Madini aina ya helium yanatumika kwa ajili ya mitambo na pia kwenye
vifaa vya matibabu kama MRI na NMR.
Kabla ugunduzi huo, watafiti walikuwa wamebashiri ukosefu wa gesi hiyo ifikapo mwaka wa 2035.
Mnamo
mwaka 2010, mwanasayansi ambaye alikuwa mshindi ya Tuzo la Nobel,
Robert Richardson alitabiri kumalizika kwa gesi hiyo katika kipindi
kifupi. Ukosefu huo ulikuwa umesababisha wataalamu, kuhimiza kutungwa
kwa sheria itakayopunguza matumizi yake katika bidhaa zisizo za dharura.
Mtaalamu
kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Chris Ballentine alisema gesi hiyo
iliyopatikana nchini inaweza kujaza silinda za gesi milioni 1.2 za
mashine za MRI.