Jeshi la Polisi mkoa Kilimanjaro jana liliwatawanya wahitimu wa vyuo
vikuu kupitia umoja wa Chadema (Chaso), waliokuwa wamekusanyika mjini
Moshi kwa ajili ya mahafali yao.
Dalili za ‘kibano’ hicho
zilianza kuonekana asubuhi wakati polisi na askari wa kikosi cha
kutuliza ghasia (FFU) wakiwa wamejihami kwa mabomu ya machozi,
walipozingira hoteli ya Keys inayomilikiwa na Philemon Ndesamburo.
Hoteli hiyo iliyopo maeneo ya Kwa Alfonsi nje kidogo ya mji wa Moshi,
ndipo ambako mahafali hayo ambayo yalikuwa yahusishe wahitimu 70 kutoka
vyuo vikuu vinne yalikuwa yafanyike.
Wanafunzi hao ni kutoka
Chuo Kikuu cha Mwenge (Mwekau), Chuo cha Kikuu cha Ushirika Moshi
(Mocu), Chuo Kikuu cha Masoka na Chuo Kikuu cha Tiba KCMC (KCMU Co).
Hata
hivyo, polisi wakiwa na magari yaliyokuwa yakipeperusha bendera
nyekundu, walivamia hoteli hiyo na kuwataka wahitimu hao kutawanyika kwa
amani, kwa vile mikusanyiko ya aina hiyo imezuiwa.
Mwenyekiti
wa Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha) mkoani Kilimanjaro, Dickson
Kibona alilaani tukio hilo akisema hakukuwa na sababu yoyote ya kuzuia
mahafali hayo.
“Wamezuia bila sababu yoyote na hii inakiuka misingi ya
kidemokrasia, Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa,” adai Kibona.
Kibona alidai kama isingekuwa kuhofia maslahi ya kibiashara ya
Hoteli ya Keys ambapo kulikuwapo pia watalii, wangegoma kuondoka kwa
kuwa hawakuvunja sheria yoyote ya nchi.
Mmiliki wa hoteli hiyo ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo,
alisema ndiye aliyewashauri vijana hao kutawanyika kwa amani na kuwataka
wasibishane na polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,
Wilbroad Mutafungwa alisema polisi walipata taarifa kuwa wahitimu hao
wangekuwa na mkutano wa kisiasa ambao ulijificha kwa mwavuli wa
mahafali.
“Tumewaita viongozi wao na kuwaeleza kuwa mikutano
yote ya kisiasa imezuiwa na watawanyike. Walituelewa na wakatawanyika,
lakini sisi bado tunaendelea kuimarisha doria mitaani,” alisema.
Hili
ni tukio la pili kwa wanachama wa Chaso kutawanywa na Polisi ambapo
juzi katika hoteli ya African Dream mjini Dodoma, wahitimu wa vyuo vikuu
mjini Dodoma nao walitawanywa na FFU.
Mkuu wa Idara ya Habari
wa Chadema, Tumaini Makene alisema Chadema inaendelea kuhifadhi
kumbukumbu za matukio yote yanayoendelea nchini, ili kujenga ushahidi
utakaojitosheleza pindi itakapoonekana ni mwafaka kuchukua hatua zaidi.
Alifafanua
kuwa chama hicho kinatambua hila zinazofanywa na Serikali kwa kulitumia
Jeshi la Polisi, na kuwa wanatambua amri zinazotolewa na watendaji wa
chama tawala kupitia wakuu wa mikoa na wilaya.
Alisema wanao ushahidi wa matukio yote utakaotumika muda wowote, watakapoamua kuishtaki Serikali ndani au nje ya nchi.