TANZANIA
inatarajia kufungua ubalozi wake nchini Qatar kwa lengo la kuendeleza
na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo huku
ikitilia mkazo katika sekta za gesi asilia, utalii, usafiri wa anga na
mawasiliano.
Rais,
Dk John Magufuli alisema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam alipokutana na
kuzungumza na Balozi wa Qatar nchini, Abdallah Jassim Al Maadadi.
Pamoja
na kutangaza kuufungua ubalozi wake nchini Qatar, Magufuli amemuomba
balozi huyo kufikisha ujumbe kwa Kiongozi wa Qatar, Shehe Tamim bin
Hamad Al Thani na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Qatar kwamba zipo fursa
nyingi za ushirikiano zinazoweza kufanyiwa kazi, huku akibainisha uwepo
wa gesi asilia zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 na mpango wa kufufua
Kampuni ya Ndege ya Taifa (ATCL).
“Najua
Qatar ina uzoefu katika maeneo hayo na sisi Tanzania tungependa
tushirikiane nanyi kuwekeza na kubadilishana uzoefu ili fursa hizo
zilete manufaa kwa pande zote mbili,” alisema Rais Magufuli.
Naye
Balozi Al Maadadi alimshukuru Rais Magufuli kwa nia yake ya kufungua
Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar na kuimarisha zaidi ushirikiano na
uhusiano na nchi hiyo, na ameahidi kufikisha ujumbe kwa kiongozi wa
Qatar na jumuiya ya wafanyabiashara Qatar waje kuwekeza Tanzania.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambaye pia Spika mstaafu wa
Bunge, Anne Makinda, Ikulu, Dar es Salaam.
Baada
ya mazungumzo hayo, Makinda alisema mazungumzo yao yameihusu NHIF na
kwamba amemhakikishia kuwa amejipanga kuona mfuko huo uliobeba matumaini
ya huduma za matibabu ya Watanzania unaboreshwa zaidi na dosari
zinazolalamikiwa na wanachama zinafanyiwa kazi.
0 comments:
Post a Comment