TANZANIA
inatarajiwa kuanza kutumia Kiswahili katika mikutano yote ya kimataifa
itakayowakilishwa na viongozi wake baada ya serikali kukamilisha kutuma
wataalamu watakaotafsiri lugha hiyo kwa watumiaji wa lugha nyingine
duniani.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo jana katika kipindi cha maswali ya
papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalumu, Zainabu Vulu (CCM).
Vulu
katika swali lake alihoji namna serikali inavyoenzi lugha ya Kiswahili
ambayo ilitumika na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuunganisha
Taifa na inatumiaje fursa ya kutumika kwa lugha hiyo kimataifa, kuwa
ajira kwa Watanzania.
Akifafanua
jibu lake, Majaliwa alisema tayari serikali ilishaamua Kiswahili kuwa
lugha rasmi ya kutumika serikalini na hata bungeni na sasa lugha hiyo
imekua zaidi na kuwa moja ya lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC).
Kwa
mujibu wa Majaliwa, tayari duniani kote vyuo vikuu vimeanza kufundisha
Kiswahili, hali iliyosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya walimu wa
kufundisha lugha hiyo kutoka Tanzania.
Kutokana
na uhitaji huo, Majaliwa alisema vyuo vikuu karibu vyote nchini,
vinafundisha walimu wa lugha hiyo kwa ajili ya kukidhi mahitaji hayo ya
kimataifa, lakini pia serikali inajiandaa kupeleka wataalamu wa
kutafsiri Kiswahili kwenda katika nchi mbalimbali.
Alisema
lengo la serikali kupeleka wataalamu hao katika nchi mbalimbali ni
kuwezesha viongozi kutoka Tanzania wanapokwenda katika mikutano ya
kimataifa, watumie Kiswahili na wataalamu hao watoe tafsiri kwenda
kwenye lugha nyingine za kimataifa.
Alisema
kwa sasa Tanzania imeshapeleka walimu wa lugha hiyo Burundi, Rwanda,
Uingereza na Ufaransa ambako wanafundisha lugha hiyo na kati ya lugha
kubwa za kimataifa, Kiswahili kama si lugha ya sita ni ya nane.
Naye
Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima (CCM), alimtaka Waziri Mkuu
kuangalia uwezekano wa kuruhusu wabunge kuwa wajumbe wa kamati za ulinzi
na usalama za wilaya na mikoa.
Akijibu
ombi hilo, alisema wajumbe wa kamati hizo katika wilaya, mikoa na
kitaifa, wameainishwa na Sheria ya Usalama wa Taifa kuwa ni wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama, ambao ni tofauti na mbunge ambaye ni
mwakilishi wa wananchi kisiasa.
Alisema
majukumu yao ni kuangalia hali ya usalama kwa undani, lakini sheria
hiyo haijamzuia mbunge au mwananchi yeyote, kwenda kutoa taarifa kama
ilivyotokea katika mauaji ya hivri karibuni, ambapo kamati hizo kutokana
na ushirikiano kutoka kwa wananchi, wahusika wameanza kukamatwa mmoja
baada ya mwingine.
0 comments:
Post a Comment