Licha ya uongozi wa Chadema
kutangaza kwamba umefuta mpango wa vijana wake (Bavicha), wa kuisaidia
polisi kuzuia mkutano mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwishoni mwa
wiki ijayo, jeshi hilo limeimarisha ulinzi kila kona ya mji.
Mkutano huo
unaotarajiwa kufanyika Julai 23, utashuhudia Rais John Magufuli akipokea
kijiti cha uenyekiti wa chama hicho kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya
Kikwete.
Kabla ya zuio la Mbowe, Bavicha walikuwa wameanza
kujiandikisha katika maeneo mbalimbali na kuchangisha fedha kupata nauli
ya kuja mjini Dodoma kuzuia mkutano huo huku polisi ikitangaza kupambana
nao.
Jana, polisi walifanya doria mji mzima wa Dodoma na kisha kukutana
na wamiliki wa nyumba za wageni na kuwataka wageni wote watakaofika
kwenye nyumba hizo kusajiliwa kwa vitambulisho vyao.
Tukio hilo limekuja
siku chache baada ya kukamatwa kwa viongozi wa Bavicha ambao jana
walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Dodoma kusomewa mashtaka na baadaye
kuachiwa kwa dhamana wakidaiwa kukutwa na maandishi ya uchochezi kinyume
na kifungu cha 32 (2) cha Sheria ya Magazeti, sura namba 229
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Waliofikishwa mahakamani ni
Mwenyekiti wa Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Mkuu Julius Mwita,
Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya, George Tito na Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji, Joseph Kasambala.
Akisoma mashtaka yao mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Lina
Magoma alidai kuwa washtakiwa watatu; Katambi, Mwita na Tito walikutwa
katika Baa ya Capetown mjini hapa Julai 8 wakiwa na fulana zilizoandikwa
lugha ya uchochezi.
Alinukuu maneno yaliyoandikwa katika fulana hizo
kuwa ni “Mwalimu Nyerere: Demokrasia inanyongwa na Dikteta Uchwara.”
Alisema upelelezi unaendelea na kwamba hakuwa na pingamizi na dhamana.
Kasambala alifunguliwa jalada lake pekee licha ya shtaka lake kufanana
na wenzake, tofauti ikiwa mahali alipokamatiwa na ujumbe huo kwenye
fulana aliyokuwa ameivaa.
Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana, Kasambala
alisema mshtakiwa huyo alikutwa katika Kituo cha Polisi cha Kati Julai 9
akiwa amevaa fulana yenye maandishi; “Mwalimu Nyerere: Demokrasia
inanyongwa.” Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na Hakimu Mfawidhi
Karayemaha, aliwapa dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi hiyo
itatajwa tena Julai 26 mahakamani hapo.
Nje ya Mahakama
Akizungumza na
wanahabari nje ya mahakama hiyo, Katambi alisema tangu walipokamatwa
Ijumaa iliyopita hawajawahi kuambiwa kosa lao.
“Tulipokuwa Capetown
tulipokwenda kula chakula walitokea askari waliovalia kiraia na kutuvuta
nje wakituambia mkuu wao anahitaji kuzungumza na sisi lakini cha ajabu
hawakutuambia kosa kwa muda wote tuliokaa ndani,” alisema.
Alidai kuwa
walihamishiwa katika rumande nyingine zilizopo Chamwino kutoka Kituo
Kikuu cha Polisi bila kuwaambia ndugu, viongozi wa chama chao wala
mawakili wanaowatetea.
Alisema katika rumande hizo kila mshtakiwa
alifungwa kwenye chumba chake. “... Sisi si majambazi lakini polisi
wametumia nguvu kubwa kutukamata na kutushikilia bila sababu ya msingi.
Lakini tuna imani Mahakama itatenda haki katika shauri hili.”
Kuimarisha
ulinzi
Jana asubuhi, polisi waliokuwa wamebeba silaha za
moto, mabomu ya machozi na mbwa walionekana wakizunguka kwa pikipiki na
magari katika mitaa mbalimbali ya mji wa Dodoma.
Msafara wa magari
zaidi ya 20 likiwamo basi kubwa lililobeba askari na gari la maji ya
kuwasha, lilizunguka katika mitaa mbalimbali kwa muda wa zaidi ya saa
mbili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema mara nyingi wamekuwa wakifanya mazoezi
ya kutembea kwa miguu lakini wakati fulani huwa wanatumia vyombo ambavyo
wamepewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.
“Leo
tumetoka kistaili ambayo pengine haijazoeleka. Hatukuwa na matembezi
ya miguu, tumetumia vyombo kwa maana ya pikipiki na magari yote
tuliyonayo. Haya ni mazoezi ya kawaida mara nyingi tunafanya doria,”
alisema.
Alisema doria hizo ni za pikipiki, miguu na magari na kwamba
yote yaliyoonekana jana ni katika kuwajenga askari kuwa tayari kwa ajili
ya kukabiliana na lolote litakalojitokeza akisema hayo ni mazoezi ya
kawaida na kwamba waliojitokeza ni maofisa wa polisi, wakaguzi, askari
wa vyeo vya juu na vya chini.
Alisema aghalabu wanafanya mazoezi hayo
usiku lakini kwa jana waliona wayafanye asubuhi ili kuwawezesha wakazi
wa Dodoma kujivunia chombo chao cha polisi.
Alipoulizwa kuhusu kauli za
mitaani kuwa mazoezi hayo ni ishara kuwa wanaogopa vijana wa Chadema,
Mambosasa alisema polisi hawaogopi mtu yeyote.
“Kwanza ijulikane
tunafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi, sheria, kanuni, mwongozo na
taratibu zote zinazoongoza nchi. Kwa hiyo tunachokifanya si mambo mapya
ni yale yaliyopo kisheria,” alisema.
Alisema polisi hawaogopi wahalifu
wa aina yoyote hata wa kutumia silaha na wamejipanga kukabiliana nao.
“Na niwaambie tu... haogopwi mtu hapa, sisi tunasimamia sheria kwa
kuwaelimisha watii sheria bila shuruti na wale wachache wasiotii
tutawashurutisha,” alisema.
Alisema wale wote wanaosema watafika Dodoma
kulisaidia jeshi la polisi watawashurutisha kwa kutumia nguvu kidogo tu
ili warudi kwenye mstari.