Watu
watatu wanaosadikiwa kuwa vinara wa kutengeneza vyeti bandia pamoja na
nyaraka mbalimbali za Serikali wamekamatwa eneo la Buguruni wakiwa na
mitambo yao.
Kukamatwa
kwao kulitokana na msako mkali uliofanywa na Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam hivi karibuni na hatimaye watuhumiwa walinaswa
wakiwa nyumbani wanakoishi eneo la Buguruni Ghana wakitengeneza nyaraka
bandia.
Kamanda
wa kanda hiyo, Simon Sirro aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni
Ashraff Maumba (37) mkazi wa Buguruni Ghana, Mwamba Seif (38) mkazi wa
Mnyamani, na Mahmudu Zuber (24) mkazi wa Buguruni.
Sirro
aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Julai 8, saa 4.00 usiku
walifanya upekuzi katika nyumba wanayoishi na kukuta nyaraka mbalimbali
vikiwamo vyeti bandia vya kidato cha nne 50 na vyeti vya vyuo vya
uuguzi.
Kamanda
huyo alisema nyaraka nyingine bandia zilizokamatwa ni stika 20 za
Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), vyeti vya
kuzaliwa 10 na vya Chuo cha Ufundi (Veta).
Nyaraka
nyingine zilizokamatwa, kwa mujibu wa Sirro ni leseni za biashara,
stika 100 za bima za magari, mitambo na vivuli 10 bandia vya vyeti vya
Chuo cha Biashara (CBE).
Katika upekuzi huo pia walikamata mihuri mbalimbali ya ofisi za Serikali na binafsi ukiwemo muhuri wa Bibi na Bwana.
“Tulifanikiwa
kukamata vifaa mbalimbali vya kutengenezea nyaraka zikiwamo karatasi
maalumu zilizo na nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya
kutengeneza zaidi ya kadi 500 za vyombo vya moto, kompyuta nne na
mashine moja ya kuchapisha,” alisema Sirro.
Kamanda
Sirro alisema watuhumiwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi huku
upelelezi ukiendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani ili kujibu
mashtaka yanayowakabili.
Katika
hatua nyingine, Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo alisema
Serikali haitakubali kuhujumiwa na watu wachache hivyo itachukua hatua
kali kwa wote wanaojihusisha na utengenezaji vyeti bandia vya Serikali.
“Tunashukuru
jeshi la polisi kuibua shina ambalo lilikuwa linatusumbua sana kutambua
ni wapi wanatengeneza vyeti hivi vya bandia na tumepata taarifa za
mawakala wanaofanya ujanja huo,” alisema Chibogoyo.