WAZIRI
Mkuu wa India, Narendra Modi anawasili leo nchini kwa ajili ya ziara ya
kitaifa ya siku mbili kwa lengo la kudumisha ushirikiano katika sekta
mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga alisema Modi
atatumia fursa hiyo kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya nchi hizi
mbili pamoja na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano wa kiuchumi.
Alisema
Modi atakutana na Rais John Magufuli Ikulu na kufanya naye mazungumzo.
Pia kuweka saini kwenye mikataba mbalimbali ya ushirikiano kati ya sekta
za viwanda, maji, elimu, sayansi na teknolojia na baadaye kuzungumza na
waandishi wa habari.
Dk
Mahiga alisema Modi pia atazungumza na jumuiya ya wafanyabiashara
wakubwa wa India ambao baadhi yao wameshaonesha nia ya kuwekeza katika
sekta ya ujenzi wa viwanda vya kutengeneza chuma, saruji, dawa ya
binadamu na maji ya matunda.
“Natoa
mwito kwa wafanyabiashara mbalimbali hapa nchini watumie fursa hii
kushiriki ili waweze kukutana na wenzao, Kongamano hilo litafanyika
kwenye ukumbi wa Benki Kuu (BoT) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakuwa
mgeni rasmi,” alisema.