test

Sunday, July 10, 2016

EURO 2016: Fainali- Nani Atanyakua Kombe leo? Utabiri Na Mambo Yote Muhimu Unayohitaji Kuyafahamu

Euro 2016 Final-France Versus PortugalHatimaye michuano ya Euro 2016 (Kombe La Mataifa Ya Ulaya La Soka) iliyoanza tarehe 10 Juni 2016 inafikia ukingoni Jumapili hii tarehe 10 Julai, 2016 kwa mchezo wa fainali kati ya wenyeji Ufaransa dhidi ya Portugal (Ureno). Kwa saa za Afrika Mashariki kipyenga kitapulizwa mida ya saa nne usiku.
Refarii ambaye amepangwa kuchezesha mechi hii ni  muingereza Mark Clattenburg (41) anayechezesha English Premier League(EPL). Huyu ndio refa aliyechezesha pia fainali ya Kombe La Klabu Bingwa Ulaya (UEFA Champions League) kati ya Real Madrid na Atletico Madrid tarehe 28 Mei jijini Milan, Italy.
Vituo mbalimbali vya Televisheni na hususani DStv (MultiChoice) vitarusha matangazo ya moja kwa moja ya mpambano wa fainali. Mpambano huu utafanyikia jiji Paris katika viungwa vya Saint-Denis katika uwanja maarufu wa Stade De France. Huu ndio uwanja ulioshuhudia Ufaransa wakinyanyua Kombe La Dunia katika fainali za mwaka 1998 walipoichapa Brazil 3-0 katika mchezo wa fainali.
Kama unafuatilia masuala ya soka, bila shaka unakumbuka baadhi ya mechi, matukio na jinsi Ufaransa na Ureno zilivyoofikia hatua hii ya kilele cha michuano. Kama hukumbuki, naomba nikukumbushe kidogo.
Safari ya timu hizi mbili kufika hatua ya fainali haikufanana. Ufaransa wameingia fainali wakitokea Kundi A. Huko walishinda 2-1 dhidi ya Romania, wakashinda 2-0 dhidi ya Albania, wakaenda sare ya 0-0 dhidi ya Switzerland. Wakatinga hatua ya makundi. Katika hatua ya makundi waliifunga Ireland goli 2-1 na kutinga robo fainali ambapo waliifunga Iceland goli 5-2. Katika Nusu Fainali wakaifunga Ujerumani goli 2-0.

Mark Clattenburg-Refa atakayechezesha fainali ya Euro 2016 kati ya Ufaransa na Ureno
Mark Clattenburg-Refa atakayechezesha fainali ya Euro 2016 kati ya Ufaransa na Ureno
Kwa upande wa Portugal(Ureno) safari yao ilikuwa ya kusuasua. Mashabiki wengi wa soka hawaamini wala kuelewa wamefikaje fainali. Mimi ni mmojawapo. Lakini soka ni mchezo ambao, kama ilivyo kwenye michezo mingine, bahati inahusika japo kidogo.Naamini Portugal wana bahati. Mtaani tunaweza kusema zali lipo upande wao katika michuano ya mwaka huu.
Wao wamefika hapa wakitokea Kundi F. Walianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Iceland. Kisha wakatoka sare ya 0-0 dhidi ya Austria na kumaliza kwa sare ya 3-3 dhidi ya Hungary. Walimaliza wakiwa namba 3 kwenye kundi.
Katika hatua za makundi wakaifunga Croatia goli 1-0 kwa goli la Ricardo Quaresma katika dakika za nyongeza. Katika robo fainali wakakutana na Poland. Hadi dakika 120 ngoma ilikuwa 1-1. Mikwaju ya penati ikaamua mshindi. Portugal wakasonga mbele kwa penati 5-3. Katika mchezo wa nusu fainali walikutana na Wales. Wakajipatia ushindi wao wa kwanza wa ndani ya dakika 90 za kawaida kwa kuwalaza Wales 2-0.
Unaweza kuona kwamba kama isingekuwa utaratibu mpya wa UEFA wa kupeleka mashindanoni timu 24 badala ya 16, bila shaka Ureno wangeshasahau kama walishiriki. Kimkandamkanda wakaingia kama timu bora ya tatu. Lakini waswahili tunasema yaliyopita si ndwele. Wameshatua fainali.
Katika historia kuanzia mwaka 1975, Ufaransa wamekutana na Ureno zaidi ya mara kumi. Katika mipambano hiyo yote Ufaransa wameshinda. Hapo ni tangu Christiano Ronaldo hajazaliwa.
Stade De France-Uwanja utakapofanyikia mchezo wa fainali kati ya wenyeji Ufaransa dhidi ya Ureno
Stade De France-Uwanja utakapofanyikia mchezo wa fainali kati ya wenyeji Ufaransa dhidi ya Ureno
Kama historia ni jambo la kuaminika na kutegemewa basi Ufaransa wanayo nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa mwaka huu. Kwanini? Mbali ya kuwa wameshawageuza Ureno “vibonde” wao, historia inayonyesha kila wanapoandaa michuano mikubwa huishia kuwa mabingwa. Walipoandaa michuano kama hii mwaka 1984 waliibuka washindi. Walipoandaa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1998, waliibuka mabingwa.
Kila mchezo huwa na nyota wake. Kwa Ufaransa na Ureno kuna wachezaji wawili ambao dunia itakuwa ikiwatazama. Wote wanacheza katika La Liga. Kwa upande wa Ureno, Christiano Ronaldo. Ufaransa wanaye Antoine Griezman anayechezea Atletico Madrid.
Mpaka sasa Antoine Griezman ndiye anayeongoza kwa ufungaji wa mabao akiwa na magoli 6. Christiano Ronaldo ana magoli 3. Hata hivyo Ronaldo ameweka rekodi ya kumfikia mfaransa Michél Platini kwa kuwa na idadi sawa ya magoli. Wote wana magoli 9 ambayo ni rekodi katika michuano hii ya Ulaya. Bila shaka Griezman atakuwa na hamu ya kuiongoza Ufaransa kwenye ubingwa na kuwa mshindani katika Ballon D’or. Christiano ambaye alishafika katika hatua hii mwaka 2004 na kupoteza dhidi ya Ugiriki atakuwa na hamu ya kuondoa lile balaa.
Mwezi Mei, Ronaldo na Griezman walikutana jijini Milan katika mpambano wa Real Madrid na Atletico Madrid. Hakuna aliyezifumania nyavu mpaka kwenye matuta. Ronaldo aliibuka na kicheko mwishoni. Real Madrid wakaibuka mabingwa. Hali ni tofauti nchini Ufaransa. Hawachezei vilabu.Wanapambana wakiwa na timu zao za taifa. Na Ufaransa watakuwa wakisindikizwa na mamilioni ya mashabiki wao.
Utabiri wangu ni kwamba Ufaransa itachukua Kombe. Nimewaunga mkono katika safari yao hii tangu mwanzo. Naamini advantage ya uwanja wa nyumbani ni kubwa. Sio rahisi waruhusu kombe liondoke. Lakini mpira ni dakika 90. Mpira unadunda. Lolote linaweza kutokea.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU