Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameeleza
kuwa fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo zitatolewa mara baada ya
kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa wanafunzi waliombewa fedha hizo toka
vyuo mbalimbali hapa nchini.
Prof.
Ndalichako aliyasema hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya
ucheleweshwaji wa fedha hizo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Kuna
zaidi ya wanafunzi 2,736 hewa ambao majina yao yamewasilishwa Tume ya
Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kulipwa fedha za mafunzo kwa
vitendo, yakiwemo majina ya wanafunzi waliofariki na waliofukuzwa chuo,” alifafanua Prof. Ndalichako.
Aliendelea
kwa kusema kuwa, kuna chuo ambacho kilituma ripoti ya wanafunzi
waliofukuzwa chuo mwaka 2013/2014 lakini majina hayo yametumwa tena kwa
ajili ya kupewa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa mwaka huu.
Kutokana
na kasoro zilizojitokeza katika majina ya wanafunzi wanaotakiwa kupewa
fedha kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo Prof. Ndalichako amesema kuwa
Serikali haitatoa fedha mpaka uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa kupata
fedha hizo utakapo kamilika kwa vyuo vyote nchini.
Aidha,
Mhe. Ndalichako amesema kuwa majina ya wanafunzi hao hewa yamewekwa
katika mitandao wakitakiwa kujihakiki TCU ili kujiridhisha kama kweli ni
wanafunzi na wanaendelea na masomo.
Vile
vile, Prof. Ndalichako amevitaka vyuo vikuu kutoa ushirikiano kwa timu
zilizotumwa katika vyuo vyao kufanya uhakiki wa wanafunzi wanaotakiwa
kupata fedha hizo kwani kuna baadhi ya vyuo vimekuwa havitoi ushirikiano
kwa kisingizio cha kuwepo kwenye mitihani.
Aliongeza
kwa kusema kuwa, vyuo kutotoa ushirikiano kwa timu zilizotumwa kufanya
uhakiki wa wanafunzi hao kutazidi kuchelewesha fedha hizo kutoka mapema.