Serikali itaanza kutumia mfumo
wa uagizaji wa pamoja wa nishati ya gesi ya kupikia (LPG), kama
inavyofanyika kwa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta taa ifikapo
Septemba mwaka huu.
Akizungumza wakati wa semina ya wadau wa sekta ya
mafuta kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Petroli wa Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Godwin Samuel alisema mpango huo
utasaidia kupunguza gharama na bei ya gesi hiyo inayoanza kutumika kwa
kasi majumbani.
Samuel alisema mpango huo pia utaongeza udhibiti wa
mapato ya Serikali katika sekta hiyo inayoshika kasi nchini.
Kuhusu
uagizaji wa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta ya taa,
Mkurugenzi huyo alisema mchakato unaendelea kuboresha mfumo wa sasa kwa
kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau yatakayotumika kubadilisha
taratibu zilizopo ifikapo Novemba, mwaka huu mikataba ya sasa
itakapomalizika.
“Tunakusudia kuongeza ushindani wenye tija katika
uagizaji wa pamoja wa mafuta ya ndege, petroli, dizeli na mafuta taa kwa
kuongeza idadi ya kampuni kulinganisha na kandarasi zilizopo
zinazofikia kikomo ifikapo Novemba mwaka huu,” alisema Samuel.
Kuhusu
elimu kwa wadau, Mkurugenzi huyo alisema Ewura inalenga kuwawezesha
kujua na kuzingatia mabadiliko yanayotokea katika sekta na biashara ya
mafuta ili kuwezesha kila upande kutimiza wajibu kulingana na sheria,
kanuni na taratibu.
“Changamoto zinazoikabili sekta na biashara ya
mafuta hayawezi kutatuliwa na Ewura pekee bali ni kwa ushirikiano wa
wadau wote,” alisema.