Wakati Mkutano Mkuu wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) unatarajiwa kujadili ajenda kadhaa ikiwamo ya
Rais John Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa chama ngazi ya taifa, baadhi
ya wajumbe wameanza kupika zengwe kutaka baadhi ya viongozi wa Zanzibar
watimuliwe.
Katika mkutano huo uliopangwa kufanyika Julai 23, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kumkabidhi kijiti hicho Rais Magufuli ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa chama hicho viongozi kukabidhiana nafasi hiyo kabla ya kumaliza muda.
Marais wastaafu wamekuwa na utamaduni wa kumwachia nafasi ya uenyekiti
wa chama Rais aliyeko madarakani kabla ya muda wao wa miaka mitanio
kumalizika, kama alivyofanya Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Makabidhiano ya kijiti hicho yatawezekana tu baada ya Rais Magufuli
ambaye atakuwa mgombea pekee wa uenyekiti kupigiwa kura nyingi za ndiyo
na wajumbe mkutano huo mkuu na hivyo chama kuandika historia nyingine
kwa Kikwete kung’atuka katika uongozi wa chama.
Hata hivyo, habari
zilizotufikia jana zinasema mbali ya ajenda ya kubadilishana
kijiti cha uongozi na kupokea taarifa ya hali ya siasa na mabadiliko ya
muundo wa chama, mikakati inasukwa ili baadhi ya viongozi wa
sekretarieti ya chama kutoka Zanzibar akiwemo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar
Vuai Ali Vuai, wang’olewe kwa kukitelekeza chama.
Habari hizo zinasema
Vuai ni miongoni mwa viongozi ambao mwaka 2014 walijikita zaidi katika
Bunge Maalum la Katiba (BMK) mjini Dodoma kwa zaidi ya miezi minne (siku
130) na kuacha kufanya shughuli za chama jambo lilosababisha upinzani
kutumia nafasi hiyo kujikita zaidi ndani ya visiwa hivyo.
“Sasa ndani ya
chama kuna fukuto, inasemekana kuwa kitendo cha wanachama hao kujikita
katika Bunge Maalumu la Katiba lililofanyika mwaka 2014 kilisababisha
matokeo mabovu ndani ya chama kwa upande wa CCM Zanzibar hivyo
inaonyesha wazi Naibu Katibu Mkuu ameshindwa kutimiza wajibu wake hivyo
ni lazima wawajibishwe,” kilisema chanzo cha habari hizo.
Bunge hilo
lililotarajiwa kukamilisha kazi kwa siku 70, lilianza Februari 18
lakini hadi Aprili 25 lilikuwa halijakamilisha na ndipo liliongezewa
siku 60 kuanzia Agosti 5 hadi Oktoba 4. Vuai alikuwa miongoni mwa
wajumbe 201 nchini ambao hawakuwa wabunge.
Kiongozi huyo alipoulizwa
kama anajua kwamba anashutumiwa na wenzake kwa madai ya kukitelekeza
chama hadi kikawa na wakati mgumu wakati wa uchaguzi mkuu, Vuai alisema
anajua na kwamba mizengwe hiyo inasukwa na kikundi cha watu wasiozidi
15.
“Suala la kwenda Bunge Maalumu la Katiba mimi kwangu siyo news
(habari). Wanaoeneza taarifa hizi nawajua na hawapendi mimi niwe katika
nafasi hii kutokana na maovu yao wanayoyafanya,” alieleza Vuai.
“Hili
suala la mimi kwenda Bunge Maalumu la Katiba linawauma na kuwakereketa
rohoni kikundi fulani... Nilishasema huko nyuma mimi sikujipendekeza
kwenda katika bunge hilo, bali nilifuata tarataibu zinazotakiwa.”
Vuai
alilisisitiza kuwa yeye kama kiongozi alifanya kazi kwa mujibu wa katiba
ya chama na madai ya uchaguzi wa Zanzibar kuwa mgumu alisema suala hilo
limeshatolewa ufafanuzi na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC), Jecha Salim Jecha.
Alisema anachojua CCM wana utaratibu wa
kubadilisha viongozi baada ya kipindi fulani, hivyo kama viongozi wake
wakuu watamwona anafaa kuendelea nafasi hiyo ataendelea kama kawaida na
endapo wataona hafai kuendelea yuko radhi nafasi hiyo ichukuliwe na
mwingine.
“Kama nitaendelea Inshallah. Lakini nafasi ya unaibu sikuomba,
sitokuja kuiomba na siwezi kuing’ang’ania ila najua kuna kikundi hapa
Zanzibar kinanifisidi kwa kujipendekeza kwa viongozi na kuongea uongo
juu yangu,” alisema.
“Nawaambia hivi, mimi sina tabia ya kujipendekeza
nafanya kazi kwa uadilifu kwa mujibu wa Katiba ya chama. Hili ndilo
linawaumiza na kueneza chuki dhidi yangu lakini hawanitishi kwa hilo kwa
sababu CCM Zanzibar si Vuai,” alieleza.
Vuai alisema kikundi hicho ni
cha wanaCCM wa Zanzibar na hakizidi watu 15 na kimekuwa na tabia ya
kufanya mambo ya kifisadi kuanzia ndani ya chama hadi kwenye jumuiya za
chama na muda ukifika atakitaja hadharani na matendo wanayoyafanya dhidi
ya CCM.
“Narudia tena muda ukifika nitawaumbua hadharani. Najua
hawanipendi kwa sababu najua ufisadi wao. Mimi sitorudi nyuma na msimamo
wangu wa kufanya kazi kwa uadilifu kwa sababu sikupata nafasi hii kwa
ufisadi,” alisisitiza.
Habari zaidi zinasema kuwa sekretarieti ya chama
hicho kwa sasa inatumia muda mrefu kubuni muundo mpya wa kuirejesha CCM
kwenye ushindani ili iweze kukabiliana vilivyo na joto la vyama vingine
vya upinzani vinavyoelekea kuwa na ushawishi mkubwa hasa kwa vijana.
Katika muundo huo, viongozi mbalimbali wanatajwa kutolewa katika
nyadhifa zao akiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ambaye kwa
sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.
Kwenye
mabadiliko hayo, Rais Magufuli anatajwa kujielekeza kwanza kwenye
Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo kwa mfumo wa chama
hicho ndiyo injini ya mwelekeo na mafanikio ya chama kwa jumla.