test

Tuesday, July 19, 2016

Makonda: Mashoga wanataka kuniangamiza

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema tangu alipotangaza kuanza kukamatwa kwa mashoga, amebaini kuna mkakati unawaohusisha watu hao zaidi ya 150 kutaka kumwangamiza.

Kauli hiyo aliitoa jana Dar es Salaam baada ya kumaliza mahojiano katika kituo cha redio Clouds FM, ambako alikuwa akifafanua hoja na changamoto mbalimbali za mkoa wake.

Alisema kuwa baada ya kubainika kwa mipango hiyo, mashoga wanane wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi.

“Lazima watu wajue jitihada na harakati za kusimamia katiba na usawa hapa nchini. Hakuna anayezipenda, vita inakuwa kubwa… Nimebaini kuwa mashoga zaidi ya 150 waliketi katika baa moja Kinondoni wakipanga njama za kunimaliza kwa namna moja ama nyingine, lakini kutokana  na taarifa za kiintelijensia, watu kadhaa, wengi wao wakiwa ni mashoga wameshakamatwa,” alisema Makonda.

Katika hatua nyingine, Makonda aliwatolea uvivu watu wanaosambaza ujumbe wa tofauti juu ya maagizo yake katika mitandao ya kijamii, ikiwamo kutengeneza akaunti feki.

“Kwanza wanapaswa kujua kuwa sina akaunti ambayo inaanza na cheo changu, hivyo akaunti zote zangu zimeandikwa kwa jina langu Paul Makonda si vinginevyo, hivyo kila mtu anapaswa kuwa makini na hilo,” alisema Makonda.

Aliweka wazi kuwa kuna agizo batili lililowekwa katika mitandao ya kijamii, akidaiwa kusema kuwa watu wasiokuwa na kazi watakwenda jela, lakini ukweli ni kwamba ameagiza wenyeviti wa Serikali za mtaa kuhakikisha kuwa wanafanya uhakiki wa wakazi wao nyumba kwa nyumba kwa ajili ya usalama wa maeneo wanayoishi.

Aidha Makonda alisisitiza kuwa kutokana na matatizo yaliyopo, kamwe Hatoacha kupambana na mafisadi katika halmashauri zote tatu za mkoa wake, pamoja na wauza unga, wafanyabiashara wa shisha na mashoga.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU