MKURUGENZI
Mtendaji wa makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL
Group), Mohammed Dewji, ameungana na matajiri wakubwa duniani, kutangaza
azma ya kugawa nusu ya mali zake kusaidia jamii.
Taarifa
kutoka mtandao mashuhuri duniani wa Forbes, imesema kuwa Dewji, ambaye
ni bilionea kijana kuliko wote barani Afrika, ameingia katika kundi la
matajiri hao ambao wametoa ahadi ya kutoa nusu ya mali zao, kusaidia
jamii.
“Baada
ya kushuhudia umasikini mkali wakati nikilelewa, siku zote nimekuwa
nikijisikia kuwajibika kutoa kwa ajili ya jamii yangu,” amesema Dewji katika barua yake ya kutangaza ahadi hiyo, ambayo ameiweka wazi kwa waandishi wa habari.
Alishukuru
wazazi wake kwa kumuunga mkono na kumjengea moyo wa kusaidia jamii na
kipekee katika wajibu wake kwa dini yake ya Uislamu wa kutoa na kujali
wahitaji na jamii.
Bilionea
huyo anakuwa Mtanzania wa kwanza kuungana na matajiri duniani, Bill
Gates na Warren Buffett katika kutangaza nia hiyo tangu 2010 na kushauri
watu wengine wenye uwezo kujitolea kwa ajili ya jamii.
Kundi
la matajiri waliokwisha kutangaza nia hiyo ya kutoa sehemu ya mali zao
kwa jamii, limeshafikia 155 kutoka nchi 17, ambapo Juni mwaka huu, kundi
hilo linalotambuliwa kwa jina The Giving Pledge, lilitangaza kupata
wajumbe wapya 17.
Wajumbe
wa mwanzo wa kundi hilo ni pamoja na Eli Broad na mkewe Edythe, John
Doerr na mkewe Ann pamoja na mmoja wa wamiliki wa Facebook, Mark
Zuckerberg na mkewe, Priscilla Chan.
Mtandao
mashuhuri wa Forbes, umemkadiria Dewji kuwa anamiliki mali zenye
thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.1, akiongoza kundi la makampuni ya
METL nchini Tanzania, linalojihusisha na biashara za viwanda vya nguo,
vinu vya unga na viwanda vya mafuta ya kula, huku kinywaji chake cha Mo
Cola, kikiuzwa bei rahisi kuliko kununua Coca-Cola.