Kufuatia
kuachiwa huru kwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi na Katibu wa
Chadema Nyanda ya Juu Kusini, Emmanuel Masonga kutoka Gereza la Ruanda,
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, amesema bado hawajafahamu ni
taratibu gani zimetumika kuwaachia huru wakati kifungo chao kilikuwa
bado.
“Katika
mazingira ya kawaida, siku yao ya kifungo walichokuwa wamepewa kilikuwa
kinaishia Juni 5, mwaka huu, lakini ghafla wakapewa taarifa kwamba
wataachiwa leo. Hatuna hakika sana ni taratibu gani zimetumika kufupisha
kifungo chao kwa sababu jambo hilo halijawekwa wazi.
“Tangu
wamewekwa gerezani ni takribani miezi mitatu, mawakili wetu walifanya
jitihada za kuhakikisha rufaa yao katika mazingira ya dharura
inasikilizwa, lakini haikuwahi kupata jaji wala kusikilizwa kwa sababu
kila jaji aliyepangiwa kesi hiyo alionekana ana udhuru,”alisema Mbowe.
Aidha,
amesema wao wanaamini kesi hiyo haikuwa ya haki kwa sababu watuhumiwa
walinyimwa dhamana mwanzoni, na kutokana na mazingira ya kesi yenyewe
hawakutakiwa kupewa kifungo.
Pia amedai kwamba wataendelea na rufaa yao ili kuweka rekodi sawa na kudhihirisha kwamba Sugu na Masonga hawakuwa na makosa.
Sugu
na Masonga walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela
Februari 26 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa
lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara
walioufanya Desemba 30 mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini
Mbeya.
Wawili hao wameshatumikia adhabu hiyo kwa siku 73 ikiwa ni zaidi ya robo ya kifungo chao.
0 comments:
Post a Comment