test

Thursday, July 28, 2016

Picha ya Mtanzania anayeteswa na Mchina yampeleka Mwigulu Geita

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amewasili mkoa wa Geita kwa ziara ya kikazi, kubwa ikiwa ni kufuatia taarifa za mateso na mauaji yaliyodaiwa kufanywa na raia wa China wanaomiliki sehemu ya mgodi wa Nyamhuna uliopo Katoro, Geita dhidi ya wafanyakazi/vibarua ambao ni Watanzania.

Takribani wiki moja sasa kumekuwa na  hali ya sintofahamu dhidi ya picha zinazoenezwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari zikionesha raia wa Tanzania anayefanya kazi kwenye mgodi tajwa akiteswa na kufanyiwa vitendo ya kinyama na mwajili wake ambaye ni raia wa china.

Ilimlazimu Waziri mwenye dhamana na usalama wa raia na mali zao kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani  ya Nchi kufika eneo la mgodi kujiridhisha kwa taarifa zilizotapakaa na kubeba simanzi kwa Watanzania.

Mwigulu Nchemba amejiridhisha kuwa kulikuwepo na tukio hilo la Mtanzania kuteswa na mwajiri wake, kipigo kilichosababisha kupoteza fahamu na siyo kifo.

Hatua za awali Waziri Nchemba alizozifanya ni kwenda gereza la Geita mjini alikohifadhiwa kijana huyo kwa madai ya kushitakiwa na mwajiri wake kwa kosa la wizi lililosababishwa apigwe.

Katika mahojiano ya Waziri Mwigulu Nchemba na kijana huyo, Mwigulu alibaini kuwa kijana huyo aliyepo gerezani ndiye mhusika hasa wa tukio lile kwa uthibitisho wa makovu yaliyopo mwili mwake na mavazi aliyovalia wakati anateswa na akiwapo gerezani.

Katika hali hiyo, ilimlazimu, Mhe. Mwigulu kwenda mgodini akiwa ameambatana na kijana huyo kwa ajili ya kutambua waliofanya vitendo hivyo vya kinyama. 
Katika oparesheni hiyo, kijana aliyeteswa na kujeruhiwa aliwabaini Watanzania 5 ambao ni walinzi wa eneo hilo na Mchina mmoja walioshirikiana kumpiga, kumtesa na kumjeruhi.

Kufuatia utambuzi huo na maelezo ya wahusika, Nchemba akaagiza wahusika wakamatwe mara moja na akaondoka nao kwa hatua zaidi za kisheria.

Katika hali nyingine ya kusikitisha, Waziri Nchemba amebaini uwepo wa wahamiaji haramu raia wa China katika mgodi huo ambapo nyaraka za uhamiaji mkoa wa Geita zinaonesha raia 28 wenye vibali ndio waliruhusiwa kukaa kwenye mgodi huo, lakini katika operasheni ya kushitukiza aliyoifanya Mhe. Nchemba amebaini uwepo wa raia wa china zaidi ya 50 wanaoishi katika mgodi huo kinyume na sheria.

Hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa na timu yake ya uhamiaji kuhakikisha wote wasio na vibali wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU