Dar es Salaam.
Baada ya Rais John Magufuli kuteua wakurugenzi 187
wapya, baadhi ya wanasiasa na wanataaluma wamesema uamuzi wa kuteua makada
wa CCM kushika nafasi hizo za ukurugenzi wa wilaya utaathiri Uchaguzi
Mkuu ujao.
Rais Magufuli, ambaye alikuwa akijielezea kuwa si mwanasiasa, juzi ameteua
zaidi ya makada 30 walioshindwa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka jana,
kushika nafasi hizo. Ni wakurugenzi 65 tu waliobakizwa.
Hatua hiyo ya kuteua watendaji wa wilaya kutoka miongoni mwa makada
waliowahi kugombea uongozi wa kisiasa, umekuja siku chache baada ya Ofisi ya
Rais-Utumishi kutangaza makada wengine kushika nafasi ya makatibu tawala wa
wilaya, uteuzi ambao pia ulilalamikiwa kuwa unaingiza siasa kwenye utendaji.
“Rais anajenga mfumo wake kwa kuteua watu loyal (watiifu) kwake. Hivyo
anaandaa uchaguzi wa 2020 kwa kuweka returning officers (wasimamizi) wake na
bado atabadilisha maeneo mengi zaidi kuelekea huko,” amesema Zitto Kabwe,
Kiongozi wa ACT Wazalendo.