WAZIRI
wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema jumla ya watuhumiwa
30 wa mauaji ya vikongwe na wenye ulemavu wa ngozi (albino) nchini,
wamehukumiwa kunyongwa, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji hayo.
Dk
Mwakyembe amesema pia kuwa serikali itaendelea kutoa adhabu kali kwa
watu watakaobainika kuendelea kuhusika na mauaji ya watu hao ili
kumaliza tatizo hilo, ambalo limeipaka matope Tanzania kwa kuonekana sio
kisiwa tena cha amani. Waziri huyo alisema hayo mjini Shinyanga jana,
alipofanya ziara yake ya kikazi.
Alisema
katika miaka ya hivi karibuni tatizo la mauaji ya wenye ualbino na
vikongwe yamepungua nchini na kwamba watahakikisha wanayakomesha kwa
kutoa adhabu kali kwa wauaji.
“Tatizo
hili la mauaji ya vikongwe na albino linatutia sana doa nchi yetu
kimataifa ambayo imekuwa ikisifika kwa amani na utulivu, hivyo natoa
mwito kwa wananchi waachane na mauaji ya watu hawa wasio na hatia pamoja
na mahakama zifanye kazi kwa kutoa hukumu za haraka kwa watu
watakaohusika na mauaji hayo,” alisema Dk Mwakyembe.
Hata
hivyo, Dk Mwakyembe alisema serikali itaanza mikakati ya kujenga
mahakama za mwanzo kwa kila kata nchi nzima ili kuondoa misongamano za
kesi mahakamani na kukarabati majengo ya mahakama ambayo yamechakaa.
Aliwataka wakuu wa wilaya, waunde kamati za maadili ya wilaya.
Akisoma
taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, alitaja
changamoto ambazo zinawakabili kuwa ni uchakavu wa majengo ya mahakama,
uhaba wa mahakimu na magereza ya Shinyanga na Kahama kuwa finyu na hivyo
kusababisha mlundikano wa wafungwa.