WAZIRI
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amekemea wanaopotosha taarifa za
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika huduma za utalii.
Amesema kodi hiyo iliwekwa miaka miwili iliyopita; na serikali haina sababu ya kuwaongezea wananchi mzigo huo.
“Hata
hao wanaosema utalii umepungua kwa sababu ya kodi hiyo, watoe hizo
takwimu tuzione, watalii wanaangalia vitu vingi ikiwemo vivutio,
usalama, amani, magonjwa. Wasiotaka kulipa kodi wanawachanganya tu
wananchi...tunasisitiza kila mwananchi kulipa kodi. Tunachotaka sisi ni
Taifa lifaidike na rasilimali ambazo Mungu ametupatia,” alisema Waziri Mpango.
Dk
Mpango alisema hayo jana mjini Morogoro, wakati wa ufunguzi wa kikao
cha kazi cha wakaguzi wa ndani wa wizara, idara, wakala, sekretarieti za
mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa, iliyofadhiliwa na Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Ufunguzi huo ulikwenda sambamba na uzinduzi wa miongozo mitatu ya ukaguzi wa ndani.
Pia,
Waziri Mpango aliwataka watumishi wa umma, kufuata na kutekeleza
maagizo ya serikali, ikiwa ni pamoja na kufanyia mikutano na semina zote
katika kumbi za serikali.
Alisema
vinginevyo watachukuliwa hatua kama vile kukatwa mishahara ili kufidia
fedha za serikali wanazozitumia kulipia kumbi. Dk Mpango alisema agizo
hilo linatakiwa kutekelezwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu ili kuokoa
fedha za umma.
“Atakayekiuka
hili tutamkata mshahara wake maana watoto wanakaa chini, hospitalini
hakuna vitanda na magodoro, hakuna maji, hakuna madarasa, hakuna vyoo,
hivyo tunatakiwa kupunguza matumizi ambayo si ya lazima ili tuboreshe
sekta zingine,” alisema Dk Mpango.
Alisema
hata kama semina au mkutano unagharamiwa na wafadhili, ni jukumu la
viongozi wa umma kuwaomba kufanyia mikutano hiyo kwenye kumbi za
serikali ili fedha zinazobaki zitumike kwa kazi nyingine.
Aliwaagiza
wakaguzi wa ndani kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata miongozo ya
kitaifa na kimataifa ili kudhibiti mchwa wanaotafuna mali za umma.
Alisema
kuna hisia na madai kuhusu uadilifu mdogo wa baadhi ya wakaguzi wa
ndani na hivyo kusababisha kushindwa kutoa taarifa za vitendo vya
ubadhirifu kwa sababu nao ni sehemu ya washiriki wa vitendo hivyo.
“Natambua
si wakaguzi wa ndani wote ambao uadilifu wao unatiliwa shaka. Nafahamu
kwamba wapo waliowajibishwa kwa ajili hiyo. Hivyo naomba muongeze bidii
katika mapambano haya na serikali hatutawaonea haya wakaguzi wachache
wanaoendelea kuchafua jina la taaluma hii. Tutawachukulia hatua kali za
kinidhamu wale wote watakaokwenda kinyume na taaluma hii,” alisema.
Kwa
upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, Toshio Nagase alisema
Serikali ya Japan kupitia JICA imekuwa ikitoa msaada wa kitaalamu kwa
Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani katika kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani
tangu mwaka 2009.