Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amemteua Naibu Kamishna wa
Polisi, Maulid Makabila kuwa Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (D/DCI)
Zanzibar, huku akifanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa polisi wa
mikoa.
Kabla ya uteuzi huo, Makabila alikuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia uhalifu makao makuu ya Polisi Dar es Salaam.
Taarifa
iliyotolewa leo Alhamisi Mei 17, 2018 na msemaji wa polisi, Barnabas
Mwakalukwa imeeleza kuwa katika mabadiliko hayo aliyekuwa DCI Zanzibar,
Ramadhan Ng’anzi ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
kuchukua nafasi ya Charles Mkumbo aliyehamishiwa makao makuu ya
upelelezi, Dar es Salaam.
Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa
Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali anakwenda kuwa kamanda wa polisi Mkoa
wa Kaskazini Pemba. Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa
polisi, Thobias Sedoyeka aliyekuwa makao makuu ya upelelezi Dar es
Salaam.
“Kamanda wa polisi mkoa wa Kusini Unguja, Makarani
Khamisi amehamishiwa makao makuu ya upelelezi Zanzibar na nafasi yake
kuchukuliwa na kamishna msaidizi wa polisi, Suleiman Hassan aliyekuwa
mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kaskazini Unguja,” anasema Mwakalukwa katika
taarifa hiyo.
Aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini
Unguja, Hasina Ramadhani Taufiq anakuwa ofisa mnadhimu makao makuu ya
polisi Zanzibar na nafasi yake inachukuliwa na kamishna msaidizi, Haji
Abdallah Haji aliyekuwa ofisa mnadhimu Mkoa wa Mjini Magharibi.
Taarifa hiyo inaeleza mabadiliko hayo ni ya kawaida yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Chanzo- Mwananchi
Friday, May 18, 2018
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU
0 comments:
Post a Comment