Rais
Dkt. John Magufuli ameagiza wataalamu wote wa idara za maji katika
halmashauri zote nchini kusimamiwa moja kwa moja na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili kuimarisha usimamizi wa shughuli
zinazofanywa na idara hiyo na kuwawajibisha wahusika pale miradi
isipotekelezwa.
Rais
Magufuli pia amewataka wataalamu wa ardhi na mipango miji katika
halmashauri zote nchini kusimamiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuimarisha usimamizi wa shughuli
zinazofanywa na idara hiyo na kuwawajibisha wahusika pale mradi
unapotekelezwa visivyo.
Dkt.
Magufuli ametoa agizo hilo Mei 10, 2018 wakati alipokuwa anazungumza
mara baada ya kumaliza zoezi la kumuapisha Mhe. Alphayo Japani Kidata
kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada na Bw. Msalika Robert Makungu kuwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora na kusema hajaridhishwa na utendaji
katika sekta maji na ardhi kutokana na usimamizi mbaya wa miradi mingi
ya maji na usimamizi mbaya wa masuala ya ardhi na mipango miji.
"Sasa
hivi kila mahali watu wanalalamikia maji, Wabunge wanalalamika,
wananchi wanalalamika, serikali imetoa fedha lakini miradi haitoi maji,
ukichunguza miradi hii inasimamiwa na wahandisi wa maji wa halmashauri
ambao Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambaye ana wataalamu wa maji hana
uwezo wa kuwawajibisha, wahandisi wanawajibika kwa madiwani, sasa
hatuwezi kwenda kwa mtindo huo", amesema Rais Magufuli.
Pamoja
na hayo, Rais Magufuli ameendelea kwa kusema "kwenye ardhi kuna
matatizo mengi ya ardhi na mipango miji, watu wanadhulumiwa ardhi,
ugawaji wa viwanja ni matatizo, maafisa ardhi na mipango miji
wanachelewesha vibali vya ujenzi, huku nako Katibu Mkuu wa Ardhi na
Maendeleo ya Makazi hana mamlaka ya kuwachukulia hatua, hili nalo
tatizo".
Kwa
upande mwingine, Rais Dkt. Magufuli amemtaka Waziri wa TAMISEMI Mhe.
Selemani Jafo kukutana na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack
Kamwele na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William
Lukuvi, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi
kutengeneza muundo utakaozingatia maelekezo aliyoyatoa leo.
0 comments:
Post a Comment