Serikali
imesema hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na
virusi vya ugonjwa wa Ebola hapa nchini na kuwataka wananchi kuchukua
tahadhari kubwa dhidi ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa hivi karibuni
katika nchi jirani ya Demokarasia ya Kongo (DRC).
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Waziri
Ummy amesema kuwa hata hivyo taarifa hiyo haiizuii Tanzania kuchukua
hatua thabiti dhidi ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola kwa kuwa inapakana
na nchi ya DRC ambapo kuna mipaka mingi ambayo watu huwa wanaingia na
kutoka kwa njia zisizo za halali.
"Tanzania
imepokea taarifa ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC
uliotangazwa na shirika afya Duniani Mei 8 mwaka huu ambapo vipimo vya
maabara vimethibitisha baada ya kupokea wagonjwa 21 ambapo kati yao 17
wamepoteza maisha", amesema Waziri Ummy.
Aidha,
Waziri Ummy amewataka watu wanaoishi katika mikoa inayopakana na nchi
ya DRC kuchukua tahadhari pale wanapohisi kupata magonjwa yenye dalili
za Ebola kwa kuwahi kufika kwenye hospitali zinazotoa huduma ili
wafanyiwe vipimo vya kina kuonyesha kama wameathirika au la.
Waziri
Ummy ameitaja mikoa ambayo inapakana na nchi ya DRC kuwa ni Mwanza,
Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe na kuwataka wananchi wanaoishi
katika mikoa hiyo kuchukua tahadhari kubwa ya kujikinga na ugonjwa wa
Ebola.
“Nimeitaja
mikoa hiyo kwa sababu ina njia nyingi ambazo siyo rasmi zinazowawezesha
watu kuvuka kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine na hivyo kama
kutakuwa na mtu ambaye ameambikizwa ugonjwa huo itakuwa ni rahisi
kuusambaza tofauti na mtu nayeingia nchini kwa kutumia mipaka rasmi kama
vile uwanja wa ndege”, amesema Waziri Ummy.
Kwa
upande mwingine, Waziri Ummy amesema Wizara imechukua hatua mbalimbali
ili kudhibiti ugonjwa huo ikiwemo kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa
wa Ebola kupitia kwa makatibu tawala na waganga wakuu wote wa mikoa kwa
kujumuisha na namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa, namna ya kuchukua
sampuli na namna ya kuwahudumia wagonjwa.
0 comments:
Post a Comment