Shahidi
wa nne upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili mmiliki wa Shule ya
Lucky Vicent, Innocent Mushi pamoja na makamu mkuu wa shule hiyo,
Longino Nkana jana ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Arusha kuwa gari
lililobeba wanafunzi wa shule hiyo halikuwa na kibali cha kusafirisha
wanafunzi.
Shahidi
huyo, Allen Mwanri (48) ambaye ni ofisa mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri
wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) alisema gari hilo lilipewa leseni ya
kusafirisha abiria kutoka wilayani Arusha kuelekea Mirerani Mei 16, 2016
na kiliisha Mei 15, 2017.
Mbele
ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Desdery Kamugisha shahidi
huyo aliieleza mahakama kwamba kwa mujibu wa kumbukumbu za ofisi,
haijawahi kupokea maombi yoyote ya kubadilisha matumizi ya leseni ya
gari hilo tangu kumalizika kwa leseni yake.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi leo ambapo shahidi mwingine upande wa mashtaka atafika mahakamani hapo kuwasilisha utetezi wake.
Wanafunzi
32 wa shule hiyo, walimu wawili na dereva Mei 6, 2017 walifariki dunia
kwa ajali ya basi la shule hiyo eneo la Rhotia, Karatu mkoani Arusha
wakati wakielekea Karatu ambako watoto hao walipaswa kufanya mtihani wa
kujipima uwezo na wale wa Shule ya Tumaini.
Wakati kesi hiyo ikiendelea baadhi ya wazazi ambao watoto wao walifariki katika ajali hiyo walikuwa nje ya mahakama hiyo.
0 comments:
Post a Comment