Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Boniface Wambura (49) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
kuwa anapokea mshahara wa Shilingi Milioni 7 kwa mwezi.
Wambura
ameyaeleza hayo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya utakatishaji
fedha inayomkabili, aiyekuwa rais wa TFF Jamal Malinzi na wenzake mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Akiongozwa
na wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza kutoa ushahidi wake, Wambura
amebainisha kuwa aliwahi kuwasilisha maombi ya kutaka kuongezwa mshahara
kutoka Shilingi Milioni 2 hadi 7 wakati wa utawala wa Malinzi.
Alipoulizwa
na wakili Rweyongeza kwamba Malinzi alikataa kumuongeza mshahara,
Wambura alidai kuwa si kweli, lakini alipeleka maombi hayo tena wakati
wa utawala wa Rais wa sasa wa TFF, Walles Karia ambapo ameidhinisha
alipwe Shilingi Milioni 7 tangu August 2017 hadi sasa.
Awali
akiongozwa na Wakili wa serikali, Shadrack Kimaro, Wambura alidai kuwa
muhtasari wa June 5,2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini
wa akaunti za Benki za TFF zilizopo Stanbic ni wa kughushi na kwamba
yeye haufahamu.
Wambura
amedai anasema hayo kwa sababu alikuwepo katika kikao hicho cha June
5,2016 na hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa benki wa
TFF kwa kumtoa Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.
Baada
ya kueleza hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi May 28 na 29 , 2018 kwa
ajili ya kuendelea kusikiliza kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa
mashtaka.
Katika
kesi hiyo washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine,
Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga. Pia Meneja wa Ofisi wa (TFF),Miriam
Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya.
Kwa
pamoja washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 30 ikiwemo kula njama,
kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa
fedha wa USD 173,335 na Sh 43,100,000.
0 comments:
Post a Comment