WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania bado inahitaji wawekezaji na
kupitia kwenye uwekezaji, inapata fursa ya mitaji na teknolojia za
kisasa.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Mei 23, 2018) wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Bw. Alfayo Kidata ambaye alifika kumuaga kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkuu amemtaka Balozi Kidata atumie fursa ya uwepo wake nchini Canada
kuangalia namna ya kuisadia nchi kuimarisha sekta za kilimo, madini na
utalii.
“Tukiimarisha
sekta hizi, uchumi ndani ya nchi unakua lakini pia tunategemea kutumia
nchi rafiki kukuza uchumi wetu wa ndani kwa maana ya kukuza mitaji na
kupata teknolojia za kisasa,” amesema.
“Ukienda
huko mkakati wako mkubwa uwe ni kuzingatia mpango wa Taifa wa maendeleo
wa miaka mitano lakini zaidi mkakati wetu wa kukuza uchumi wa viwanda,”
amesisitiza.
Amemtaka
Balozi huyo akasimamie pia suala la upatikanaji wa masoko kwa ajili ya
mazao yanayozalishwa nchini ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania
waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.
“Hapa
nyumbani tuna mazao matano ambayo tumeazimia kuyafufua lakini masoko ya
ndani hayatoshi, kwa hiyo kazi yako mojawapo ukiwa huko ni kututafutia
masoko,” amesema.
Waziri
Mkuu amemweleza Balozi Kidata azingatie pia suala zima la kuongeza
idadi ya watalii. “Tunataka ukasaidie kutangaza nchi yetu ili watalii
waje kuona vivutio vyetu. Tunataka kuongeza idadi ya watalii kutoka
milioni mbili ya sasa hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2020,”
amesema.
Alimtaka Balozi huyo akafuatiilie pia fursa za masomo kwa ajili ya Watanzania wanaotaka kusoma Canada na Cuba.
“Nilipoongea na Makamu wa Rais wa Cuba, aliahidi kuongeza idadi ya Watanzania wanaotaka kusomea udaktari. Kwa hiyo, ukifika itabidi ufuatilie ahadi hiyo,” ameongeza.
“Nilipoongea na Makamu wa Rais wa Cuba, aliahidi kuongeza idadi ya Watanzania wanaotaka kusomea udaktari. Kwa hiyo, ukifika itabidi ufuatilie ahadi hiyo,” ameongeza.
Waziri
Mkuu pia alimsisitizia Balozi Kidata akifika huko awatambue na
kuwaunganisha Watanzania waishio Canada na awahamasishe wafanye kazi ili
waweze kuwekeza nyumbani.
Kwa
upande wake, akizungumza baada ya kuagana na Waziri Mkuu, Balozi Kidata
alisema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa na
Waziri Mkuu.
Alisema
anatambua kwamba Canada ina idadi ya watu zaidi ya milioni 40 na
atafanya juhudi zaidi za kuitangaza Tanzania ili waje kuona vivutio
vilivyopo nchini. Pia atafuatilia fursa za mafunzo kwa wanafunzi wa
Kitanzania.
“Kwenye
suala la uchumi wa viwanda, tunahitaji kuwa na uzalishaji wa mazao ya
kutosha. Kwa hiyo tunahitaji kuwana kilimo cha uhakika na cha muda wote
kuliko. Tunahitaji kupata utaalamu na mitaji kwa ajili ya mashamba ya
umwagiliaji,” alisema.
Alisema kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji, kutasaidia kuwe na uhakika wa upatikanaji wa malighafi zitazakotumika kwenye viwanda.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment