HATIMAYE benchi la ufundi la Klabu ya Yanga limeamua kukubali kuwa
wapinzani wao Simba kwa msimu huu ndiyo mabingwa huku wao sasa
wakijipanga kuelekeza nguvu zao katika michuano ya Kombe la Shirikisho
Afrika.
Yanga ndiyo mabingwa watetezi wa ligi kuu baada ya kuutwaa msimu
uliopita wakiwazidi Simba kwa mabao ya kufunga lakini kwa msimu huu hadi
sasa wanakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na pointi 48
ambazo ni pointi 17 nyuma ya Simba wanaongoza ligi wakiwa na pointi 65.
Akizungumza na Championi Jumatano, muda mfupi baada ya kurejea kutoka
nchini Algeruia, Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani Zahera Mwinyi alisema
kwa sasa wamekubali kuwa wapinzani wao ndiyo mabingwa wa ligi huku wao
wakielekeza nguvu sasa katika michuano ya kimataifa ambayo wanashiriki.
“Kwa hali ilivyo kwa sasa Simba ndiyo mabingwa wa ligi kwa msimu huu
huku sisi tumepanga kwa sasa kuelekea nguvu zetu katika michuano ya
kimataifa ambapo tunashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
“Tunaelekeza nguvu huko kwa sababu hapa Tanzania hatuwezi kuwa mabingwa lakini pia Kombe la FA tumeshatolewa,” alisema Zahera.
Akizungumzia juu ya mwanzo mbaya wa kikosi hicho katika mchezo wake wa
hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, Mkongomani huyo alisema:
“Tulienda na wachezaji ambao hawana uzofu na michuano hii na ndiyo
sababu iliyochangia kwetu kufungwa mabao 4-0 mbele ya wapinzani wetu,
licha ya kwamba walifuata maelekezo ya kile ambacho niliwaambia.
“Wachezaji wale muhimu tuliwaacha hapa Dar, utaona jinsi jambo hilo
lilivyoweza kuchangia sisi kupoteza mechi yetu ya huko. Nimepanga
kuongea na uongozi ikiwezekana kwamba kuwe na timu mbili ambapo moja
itaenda Mbeya kucheza na Mbeya City (kesho Alhamisi) halafu ikimaliza
iende pia Morogoro kucheza na Mtibwa.
“Wakati huohuo pia kuwe na timu ambayo nitabaki nayo hapa Dar ambayo
itajumuisha wale wachezaji ambao hawakwenda Algeria ambao nitakaa nao na
kuzungumza, hii timu nitawapa mafunzo kuhakikisha kwamba inafanya vyema
kwenye mchezo wetu dhidi ya Rayon Sport.
“Nafanya hivyo kwa sababu nataka nguvu zetu nyingi tuelekeze huko kwenye
michuano ya kimataifa kwani ndiyo nafasi pekee ambayo imebaki kwetu
kuona tunashiriki michuano ya Afrika kwa msimu ujao, kwani hakuna sehemu
nyingine zaidi ya huku hivyo yatupasa kuweka nguvu zaidi,” alisema
Mkongomani huyo.
Thursday, May 10, 2018
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU
0 comments:
Post a Comment