RAIS
John Magufuli, amelishukia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na la Magereza
kwa kutengeneza idadi ndogo ya madawati kutokana na Sh. bilioni nne
zilitolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili, mwaka
huu.
Akizungumza
wakati wa shughuli ya makabidhiano ya madawati hayo kwenye viwanja vya
Karimjee, jijini Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alieleza kushangazwa
kwake na majeshi hayo kutengeneza madawati 53,450 tu katika kipindi cha
miezi mitatu (siku 90) tangu fedha hizo zilipotolewa wakati wana nguvu
kazi ya kutosha.
Hata
hivyo, taarifa iliyotolewa jana jioni na Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa, madawati 61,385 ndiyo
ambayo yametengenezwa katika awamu ya kwanza kutokana na fedha hizo za
Bunge, ikiwa ni idadi tofauti iliyosemwa na Rais mapema kwenye hafla
hiyo.
Taarifa ya Ikulu ilifafanua kuwa, madawati mengine 60,000 yatatengenezwa kwenye awamu ya pili.
Rais
Magufuli aliongeza kuwa, ukigawa idadi ya siku 90 kwa vyombo viwili vya
JKT na Magereza, maana yake kila chombo kimetengeneza madawati 30,000.
Rais
Magufuli alisema JKT ina kambi nyingi na kutolea mfano za Oljoro,
Makutupora, Mafinga, Mpwapwa, Mlale na kwamba ukigawa kwa idadi ya kambi
hizo kwa madawati 30,000 unapata wastani wa madawati 30 kwa siku,
ambayo yametengenezwa na kila kambi.
Kutokana
na hali hiyo, amewataka wakuu wa JKT na Magereza kuchukua jukumu hilo
la utengenezaji madawati kama vita, kwa kuwatumia wafungwa na nguvu kazi
zilizopo katika vikosi kuharakisha utengenezaji wa madawati.
Katika
shughuli hiyo alikabidhi madawati hayo kwa wabunge wa mikoa ya Dar es
Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya,
Songwe, Rukwa, Katavi, Unguja, Pemba na Tanga.
Madawati
hayo yalitengenezwa kutokana na hundi ya Sh. bilioni nne iliyotolewa na
Bunge na kukabidhiwa Rais Magufuli Aprili 11, mwaka huu kama mpango wao
wa kubana matumizi.
“Natoa
wito kwa vyombo vya ulinzi, JKT na Magereza japokuwa mmetengeneza
madawati lakini mjipange katika hili, haiingii akilini, nimekaa JKT
mwaka mzima najua hamuwezi kutengeneza madawati machache hivi,” alisema Magufuli.
“Niwaombe,
chukueni hili kama jukumu la haraka, tunahitaji madawati, ninahitaji
madawati leo na Waziri Mwinyi (Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Hussein Mwinyi) yupo hapa na kwa bahati mbaya hajaenda JKT hajui
shida tunazozipata kule, labda siku mumpeleke siku akaone, sisi
tunafahamu kule ni kazi tu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema
JKT na Magereza wana nguvu kazi kubwa wakiwamo wafungwa ambao
hawahitaji fedha yoyote kufanya kazi kwani ni wajibu wao, na kwamba kila
mkoa kuna magereza hivyo askari waliopo katika magereza hayo wakafanye
kazi.
Alisema wafungwa waliofungwa katika magereza wanapewa chakula kutoka katika bajeti kuu, hivyo wanapaswa kufanya kazi.
Rais
Magufuli alisema hata fedha anazotarajia kuzipata kwa ajili ya
utengenezaji wa madawati mengine kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na PPF anasita kuvipatia
vyombo hivyo vya ulinzi na usalama kwa kuogopa kuchukua muda mrefu.
“Kama
mmeshindwa mniruhusu niwa ‘involve’ wakuu wa mikoa, nina uhakika
nikimwambia Makonda akiwahusisha vijana wa vijiweni mwezi mmoja madawati
yataisha. Sasa mnisaidie ndugu zangu makamanda mkatengeneze madawati.
Nimeona bora niongee hapa ili nisitoke na kiungulia, ila nyie ndiyo
mtoke na kiungulia,” alisema Magufuli
Rais
Magufuli alisema anahitaji madawati haraka ili kuondoa uhaba
unaozikabili shule za sekondari na msingi wa madawati 1,400,000.
Alisema
hadi sasa zaidi ya madawati 1,000,000 sawa na asilimia 88 ya madawati
yaliyohitajika kwa shule za msingi na asilimia 95.8 kwa shule za
sekondari yamepatikana.
Rais
Magufuli alisema kwa sasa kwa shule za msingi imebaki asilimia 11.2
kumaliza tatizo la madawati, huku kwa shule za sekondari imebaki
asilimia 4.2,
Alisema
tangu atoe agizo kwa wakuu wa wilaya na mikoa ya kutengeneza madawati,
halmashauri 25 zimefikia malengo kwa upande wa shule za msingi na
halmashauri 46 kwa shule za sekondari.
Katika
mgawanyo wa madawati hayo, mkoa wa Dar es Salaam ulipata madawati
5,370, mikoa mingine na idadi yao katika mabano ni Pwani (4,833),
Morogoro (5,907), Lindi (4,295), Mtwara (5,370), Ruvuma (4,833), Iringa
(3,757), Njombe (3,222), Mbeya (3,759), Songwe (3,222), Rukwa (2,285),
Katavi (2,683) Unguja (3,200), Pemba (1,800) na Tanga (6,444).
Kadhalika,
Rais Magufuli alisema baada ya kuanza kutekeleza ahadi ya kuondoa ada
kwa shule za msingi na sekondari, idadi ya wanafunzi waliojiandikisha
kuanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wanafunzi 1,282,100 hadi
kufikia wanafunzi 1,896,584 sawa na ongezeko la asilimia 84.5 hali
iliyosababisha upungufu wa madawati 1,400,000.