test

Thursday, July 14, 2016

RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi (A Wizard Student) - Sehemu ya 14

...MWALIMU John alijishangaa kupita kiasi kwani miguu yake yote miwili ilikuwa imeoza vibaya. Alikuwa hahisi maumivu yoyote hapo kabla lakini pindi alipojitizama tu alianza kuhisi maumivu makali sana. Punde funza wakaanza kutoka mguuni. Akabaki anajiuliza nini kimetokea bila kujua sababu.
Mkewe na baadhi ya ndugu zake walibaki kimya, wakimtazama Mwalimu John kwa woga.
 
"Mke wangu bado unaniogopa? Hunionei hata huruma mumeo? Ama kweli mapenzi yapo kwenye raha tu!" Alisema Mwalimu John kwa huzuni iliyochochea huruma nyingi machoni mwa mkewe. Taratibu akaanza kumsogelea mumewe lakini kuna ndugu yake mmoja akata kakumzuia.
 
"Niache! Nampenda mume wangu ingawa yupo kwenye hali hiyo.." Alisema mke wa mwalimu John huku akimsogelea mumewe kisha akamkumbatia kwa mapenzi mazito, bila kujali hali aliyokuwa nayo mumewe.
 
"Nakupenda mume wangu.. Nashukuru umeurudia uhai ili tuendelee kuwa pamoja" alisema mwanamke yule huku machozi yakimchuruzika.
 
"Nakupenda sana mke wangu, nilikuwa nakuwazia sana hali ambayo ungeikabili kama ningekufa.."
"Sijui ningemweleza nini mwanao aliyeko tumboni mwangu!" Walizungumza yote hayo wakiwa bado wamekumbatiana. Maneno ya mke wa Mwalimu John yalimfariji sana John, akahisi kwamba kweli amerudi duniani.

Ndugu walibaki wametumbua macho wakiwatazama wawili wale, hawakuwa na la nyongeza zaidi ya kumkaribisha mwalimu John ambaye hakuweza hata kutembea kutokana na maumivu ya miguu. Funza walizidi kuongezeka miguuni.
 
"Mke wangu naumwa sana hii miguu, sijui kama itapoa!"
"Usijali itapona tu mume wangu.. Ila naomba unieleze kila kitu kilichokutokea..!" Alisema mke wa mwalimu John huku akimwinua taratibu mumewe pale chini alipokuwa ameketi.
Mwalimu John alilalama sana kutokana na maumivu Yale lakini ikabidi ajikaze mpaka walipoingia ndani.
"Mke wangu Leyla.. Kweli nimeamini unanipenda!"
Leyla akatabasamu na kumbusu mumewe kisha akasema
"Nakupenda sana mume wangu hebu nisimulie imekuwaje..!"
"Ni stori ndefu sana mke wangu..lakini ngoja nikusimulie mbele ya hawa ndugu zangu wote..!"
Wote sebuleni pale walitulia kimya kusikiliza kisa cha ajabu kilichompata Mwalimu John. Lakini cha ajabu Mwalimu John alipotaka kusimulia tu..

*******
Wazazi wa Eddy walichanganyikiwa sana wakahisi mtoto wao mpendwa tayari amefariki dunia. Wakazidi kumtikisatikisa huku mama yake akiushusha mchozi kama maji, ndipo wakagundua Eddy hajafa ila amepoteza fahamu. Kofi alilopigwa halikuwa la mchezo, lilikuwa kama radi ingawa wazazi wake hawakujua kitu.
Na hiyo ilikuwa ni kazi ya mzimu unaomsaidia Doreen.

Mr.Alloyce alitumia nguvu zake zote kumpepea Eddy mpaka alipozinduka. Alikuwa amevimba USO mzima jambo lililowashtua wazazi wake. Wakatazamana kwa nyuso zilizojaa viulizo bila kujua majibu ya uhakika.
"Eddy" Mr.Alloyce aliita.
"Naam!" Eddy aliitikia kwa sauti ya chini.
"Vipi?"
"Nimepigwa!"
"Umepigwa? Umepigwa na nani?"
"Sijui!"
Yote yaliyomtokea Eddy yalibaki kuwa viulizo kwa wazazi wake, yaliibua fumbo ambalo lilikuwa gumu sana kulitatua.
"Baba Eddy"
"Sema mke wangu..!"
"Mi naona twende kwa mganga tu!"
"Wapi?"
"Tanga kwa mganga Tembo wa Bahari.. Umewahi kumsikia?"
"Mmh! Hapana..!"
"Nasikia ni kiboko sana kwani hata Mama Zuwena aliwahi kwenda akasaidiwa!"
Mama Eddy aliamua kumshauri mumewe waende kwa mganga wa kienyeji anaepatikana Pangani Tanga. Mganga Hugo alifahamika kwa jina la Tembo wa Bahari kwani alisifika kwa kutatua matatizo yaliyoshindikana lakini Mr.Alloyce alisitasita kuhusu suala hilo.
"Waganga siwaamini mke wangu..!"
"We unafikiri tutafanyaje sasa! Kama hutaki niachie kila kitu Mimi nitahangaika na mwanangu..!" Mama Eddy alilivalia njuga suala lile hatimaye Mr.Alloyce akaingia laini na kumkubalia mkewe.
"Sawa tutaenda!"
"Twende kesho!"
"Haina shida"

Walikubaliana kuianza safari yao siku ya kesho yake.

Siku ile hawakumsumbua Eddy kwa swali lolote lile, usiku aliingia kulala akiwa bado hana raha kabisa huku akiisubiri siku ya kesho yake ili waende kwa mganga.

Eddy alipojilaza kitandani tu, usingizi mzito ukampitia. Ghafla akamuona Doreen ndotoni akija na kisu kikali sana kinachowaka moto. Eddy aliogopa sana akatamani kuamka lakini akashindwa.
"Eddy ukithubutu kusema lolote kuhusu Mimi utakiona cha moto... Kubwa zaidi ukithubutu kwenda kwa mganga hiki kisu ni halali hapo kifuani pako.. Utakufa!"
Ilisikika sauti ya Doreen ikiongea kwa msisitizo sana huku ikijirudiarudia.

"Mamaaaa!" Eddy alishtuka usingizini na kumwona mama aliyekuwa amelala chumbani kwake ili kujua maendeleo ya Eddy kila wakati.
"Vipi mwanangu?" Mama Eddy alishuka kitandani na kukisogelea kitanda cha Eddy.
"Ndoto mama.. Naogopa!"
"Pole mwanangu.. Usiogope tupo wote humu..! Alisema mama Eddy lakini Eddy bado aliogopa.

Usiku ule ulikuwa mrefu sana kwa Eddy kwani alikumbana na vitisho Vinci kutoka kwa Doreen. Kulipokucha Eddy aliona ahueni kidogo ili aachane na mauza uza ya usiku.

Majira ya SAA kumi na mbili na nusu asubuhi wazazi wa Eddy walikuwa tayari wamejiaandaa. Wakamwamsha Eddy ili anywe chai kisha waanze safari, cha ajabu Eddy aligoma kuondoka.
"Siwezi kwenda kwa mganga! Siendi!"
"Huendi?" Mama Eddy alishtuka
"Siendi mama! Hata kwa greda!"
"Kwanini?"
"Sitaki!"
Eddy aligoma kabisa kuondoka lakini mama yake alimlazimisha na kumweka kwenye gari akisaidiana na baba yake. Safari ikaanza.

********
Doreen aliamua kusubiri usiku uingie ili amfuate Nadia na kumfanyia uchawi wake ili aondoke na ziwa.

Usiku ulipoingia Doreen alikuwa akijipanga kwa kuita mizimu yake yote ili imwongezee nguvu. Alikuwa amejitenga peke yake kwenye kichaka huku akijpakapaka madawa yake ili aongeze nguvu zake za kichawi. Akainuka akiwa uchi huku akijiaminisha kuwa sasa yĆ¹ kamili. Akatamka maneno yake ya kichawi akatoweka eneo lile..
Muda huo ilikuwa ni saa name usiku.

Akaenda moja kwa moja mpaka bwenini kwa Nadia na kukifikia kitanda chake, mh! Alichokutana nacho hakuamini.. Moto ilikizingira kitanda kizima na hakumuona Nadia Joseph alipo. Akaamua kukisogele kitanda kile taratibu lakini ghafla akapigwa dhoti Kali na kudondoka chini puuuh! Kama mzigo. Na kila alipojaribu kuinuka alishindwa.. Hofu ikamjia akajua tayari amekamatwa kwenye mtego....

Itaendelea....
TANGAZA HAPA KWA BEI NAFUU