Sakata
la mradi wa umeme wa Stigler’s Gorge ambao utekelezaji wake unafanyika
katika pori la akiba la Hifadhi ya Selous, liliibuka tena bungeni jana
jioni Mei 22, 2018 na kuzua mvutano huku Spika Job Ndugai akieleza
kutoridhishwa na majibu ya Waziri wa Maliasili na Utalii.
Suala
hilo lilitikisa Bunge jana mchana baada ya wabunge kadhaa kuhoji
utekelezaji wa mradi huo, kueleza athari za kimazingira zinazoweka
kujitokeza.
Selous
ni miongoni mwa mapori yanayotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa
la Elimu na Utamaduni (Unesco) kama sehemu ya urithi wa dunia, lakini
uamuzi wa Serikali kuzalisha zaidi ya megawati 2,100 ikitumia zaidi ya
Dola 2bilioni (zaidi ya Sh4.5trilioni) unaelezwa kuwa huenda ukaliondoa
pori hilo kwenye orodha hiyo.
Bunge
lilipokaa kama kamati jana jioni kupitisha bajeti ya Wizara ya
Maliasili na Utalii mwaka 2018/19 ya Sh115bilioni, mbunge wa Ulanga
(CCM), Godluck Mlinga alianza kwa kuhoji kama Serikali itakuwa na
mkakati mzuri wa kuwasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.
Hoja
ya Mlinga iliungwa mkono na Ndugai aliyeitaka Wizara ya Nishati kuwa
makini na kutengeneza utaratibu wa kupanda miti katika maeneo mbalimbali
yanayoanzishwa miradi ya umeme.
Ndugai
amesema katika maeneo mengi Wizara hiyo imekuwa na utaratibu wa kukata
miti mingi katika utekelezaji wa miradi lakini inakosa usimamizi wa
upandaji miti mingine.
“Mheshimiwa
Mlinga naamini kuwa wamekuelewa lakini na ninyi Nishati lazima muwe na
mipango mizuri ya kupanda miti katika miradi yenu. Haiwezekani unakata
miti lukuki lakini hakuna mpango wa kuipanda hiyo haikubariki kabisa,”
amesema Ndugai.
Ndugai
ambaye pia aliungwa mkono na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),
Zitto Kabwe kwa pamoja walipingana na majibu ya Waziri wa Nishati, Dk
Medard Kalemani kuhusu upandaji wa miti katika eneo hilo.
Wakati
wawili hao wakitaka kusikia majibu ya Serikali kuhusu utunzaji wa
mazingira katika eneo hilo, ikiwa ni sambamba na kupanda miti baada ya
kuikata iliyopo, Dk Kalemani hakuwa akitoa majibu ya kina kuhusu hoja
yao hiyo.
Katika
majibu yake Dk Kalemani alisema miradi inayoanzishwa itakuwa na mipango
mizuri hata ya uhifadhi wa mazingira, huku akijikita zaidi kueleza
mpango wa kuongeza nguvu ya uzalishaji umeme nchini.
“Yaani
Waziri hujatuelewa kabisa tunachotaka sisi ni hii miti mingi mnayokata
halafu mnakusanya na hampandi mingine, hivi hamjui habari ya uhifadhi
kweli basi nimemaliza, nimemaliza waziri usisimame tena,” alisema Ndugai
baada ya waziri huyo kuomba kujibu tena huku wabunge wakipinga.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola
alisema mradi huo hauna madhara kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,
akijitokeza mtu akaupinga atafungwa bila huruma.
0 comments:
Post a Comment