Mmoja
wa mawaziri walio katika Kamati ya Usalama ya Baraza la Mawaziri Israel
amesema wanaweza kuupindua utawala wa Rais, Bashar al Assad na kumuua
iwapo Iran itatumia ardhi ya Syria kuishambulia Israel.
Waziri
huyo wa Nishati, Yuval Steinitz amenukuliwa na mtandao wa habari wa
Israel, Ynet akisema Israel haijajiingiza katika vita vya wenyewe kwa
wenyewe nchini Syria hadi sasa.
Lakini
alionya iwapo Rais Assad ataendelea kuiruhusu Iran kuendesha shughuli
zake katika ardhi ya nchi hiyo Israel itammaliza na kuundoa madarakani
utawala wake.
Kadhalika
Waziri huyo ameendelea kueleza ikiwa Rais Assad atairuhusu Iran
kuigeuza Syria kambi ya kijeshi dhidi ya Israel anapaswa kufahamu huo
utakuwa mwisho wake.
Israel na Iran zimekuwa zikishambuliana katika vita maneno kuhusu Syria tangu Februari mwaka huu
Aprili
9 mwaka huu shambulio la anga liliua askari sita wa kikosi cha
makomando cha Revolutionary Guards cha Iran kambini nchini Syria.
Tehran
iliilaumu Israel na kuapa kulipa kisasi, kauli iliyojibiwa na Israeli
kuwa itafanya mashambuilizi makubwa dhidi ya miliki za Iran nchini
Syria.
Pia
Waziri Steinitz alionekana kugusia kuwa kauli yake haiakisi sera ya
Serikali ya Israeli, akisema: ‘Sizungumzii kuwapo mkakati wowote
kumhusu.”
Hakukuwa
na mwitikio wa haraka kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin
Netanyahu wala Wizara ya Ulinzi Israel kuhusu kauli hiyo nzito.
Iran,
wanamgambo wa Lebanon, Hezbollah na Urusi zimekuwa zikiimarisha
usaidizi wao kwa Damascus dhidi ya uasi wa miaka saba nchini Syria.
Lakini Israel inahofia uwapo wa maadui wake Iran na Hezbollah utatengeneza jeshi nchini humo litakalotishia usalama wake.
0 comments:
Post a Comment