Makhtar Diop, raia wa Senegal ameteuliwa kuwa makamu wa rais wa Benki ya Dunia (WB) atakayekuwa anasimamia miundombinu.
Diop
alitangazwa kushika nafasi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita na hivyo
kumfanya kuwa miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu wa taasisi hiyo
muhimu duniani.
Taarifa
iliyotolewa na benki hiyo inasema Diop anayaanza majukumu hayo mapya
baada ya kuwa Makamu wa Rais anayesimamia Afrika katika miaka sita
iliyopita akifanikisha kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya Dola 70
bilioni za Marekani.
Ndani
ya miaka hiyo sita, Diop alisimamia miundombinu ya usafiri na
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), nishati na madini, fedha
na ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP).
‘Katika
majukumu yake mapya, Diop atasimamia ufadhili wa miundombinu ya fedha
katika ufanikishaji wa maendeleo endelevu hivyo kupunguza tofauti
iliyopo kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea,” inasomeka sehemu
ya taarifa hiyo.
Uteuzi wa Diop anayetajwa kuwa miongoni mwa Waafrika 100 wenye ushawishi zaidi duniani utaanza Julai Mosi.
Alipokuwa
akiisimamia Afrika, inaelezwa alisimamia upatikanaji wa fedha za
kufanikisha miradi ya aina tofauti akihamasisha zaidi ubunifu na
uvumbuzi wa kisayansi.
Alihakikisha Afrika inapata umeme wa uhakika na nafuu huku ikiunganishwa kwa barabara zinazopitika wakati wote.
Ndani
ya benki hiyo, Diop ameshahudumu kama mkurugenzi wa fedha, sekta
binafsi na miundombinu Amerika Kusini na Visiwa vya Caribbean.
Kati
ya mwaka 2009 na 2012 alikuwa mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia,
Brazil ambako alisimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Alishawahi kuwa Mkurugenzi Mkazi katika nchi za Kenya, Eritrea na Somalia.
0 comments:
Post a Comment