Rais
wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume amemtembelea
mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro ofisini kwake akieleza
wamejadiliana mambo manne yanayohusu masuala ya sheria na haki.
Wakati
Fatma akieleza hayo jana, msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas
Mwakalukwa alisema: “Alikuja kujitambulisha kuwa yeye ni rais wa TLS.
Ilikuwa ziara ya kawaida na binafsi, hapa tunapokea wageni wa kila
aina.”
Fatma
ameyataja mambo waliyojadiliana kwakina na IGP Sirro kuwa ni wanasheria
kutobughudhiwa wanapokuwa kwenye vituo vya polisi, hali ya usafi na
usalama wa mahabusu wawapo rumande, haki ya maandamano na uhuru wa
polisi kufanya uamuzi bila kushinikizwa na wanasiasa.
Fatma
ambaye ni wakili wa kujitegemea alichaguliwa kuongoza TLS Aprili 14,
akichukua mikoba ya Tundu Lissu aliyemaliza muda wake wa uongozi.
Alisema wanasheria wamekuwa hawatendewi haki wanapokuwa katika vituo vya polisi kutetea wateja wao.
Fatma
alisema ni haki ya kila raia kuwa na mwanasheria anapopata tatizo la
kisheria na ni haki ya wanasheria kutimiza majukumu yao bila kuingiliwa.
Pia, alisema walijadiliana kuhusu usafi wa mahabusu na kutojaza watuhumiwa kwenye vyumba vidogo.
Alisema alizungumzia haki ya wananchi kuandamana na umuhimu wa kufanya hivyo.
Kuhusu
uhuru wa polisi kufanya kazi bila kuingiliwa alisema: “Natambua kuwa
sheria ya mfumo mzima wa Jeshi la Polisi haijakaa sawa, ingekuwa amri
yangu ingebadilishwa ili kuwe na usawa katika utendaji na wao wafanye
kazi zao bila kuingiliwa na wanasiasa.”
“Nchi
zilizoendelea wakuu wa polisi wanateuliwa na kamati, lakini sheria za
nchini wanateuliwa na Rais, jambo ambalo linawawia vigumu kufanya kazi
kwa kujitegemea,” alisema Fatma.
Alisema
anatambua hilo lipo nje ya uwezo wa Polisi, hivyo kitu pekee
wanachopaswa kufanya ni kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Fatma alisema IGP Sirro aliwaomba kuelimisha wananchi kuhusu sheria, kutambua haki zao na wajibu wao katika kuzitekeleza.
“Nimelichukua
hili, tutatafuta majukwaa kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii kuhusu
sheria, namna ya kuzitekeleza na wajibu wao,” alisema Fatma.
0 comments:
Post a Comment