Rais
wa Marekani, Donald Trump amepinga kauli ya mshauri wake mkuu wa
masuala ya ulinzi, John Bolton aliyedai kuwa mfumo wa kuondoa silaha za
kinyuklia nchini Korea Kaskazini utafanana na uliotumika Libya.
Tump
amesisitiza kuwa makubaliano kati ya Marekani na Korea Kaskazini
yanayotarajiwa kuanza katika mkutano kati ya viongozi wa nchi hizo
mbili, uliopangwa kufanyika Juni 12 mwaka huu hayana mlengo wowote wa
mfanano na aliyoyasema Bolton.
“Mfumo uliotumika Libya sio mfumo ambao tunaulenga tunapofikiria suala la Korea Kaskazini,” alisema Trump.
Rais
Trump alifafanua kuwa anachofikiria ni kuhakikisha Korea Kaskazini
inafuata mfumo wa Korea Kusini katika kuleta maendeleo baada ya
kuondolewa vikwazo. Aliwasifu watu wa Korea Kaskazini kuwa ni watu
wazuri na wachapakazi, hivyo anaamini baada ya makubaliano hayo
yatakayoondoa vikwazo pia nchi hiyo itakuwa tajiri zaidi.
Korea
Kaskazini ilitishia kuachana na mpango wa kiongozi wake, Kim Jong-un
kufanya mazungumzo na rais Trump nchini Singapore baada ya kukasirishwa
na kauli za Bolton pamoja na mazoezi ya pamoja kati ya Marekani na Korea
Kusini ambayo waliyataja kuwa ni mazoezi ya kujiandaa kufanya uvamizi.
Mwaka
2003, Libya chini ya uongozi wa Muammar Gaddafi ilitangaza kuachana na
mpango wake wa kutengeneza silaha za maangamizi za kinyuklia, hatua
iliyoishtua dunia. Uamuzi huo ulisababisha kuondolewa vikwazo pamoja na
kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Marekani pamoja na
washirika wake.
Hata
hivyo, mwaka 2011, Libya ilivamiwa na waasi walioungwa mkono na
Marekani chini ya mwamvuli wa NATO na mwisho wakamuua Gaddafi.
Historia
hiyo imemshtua Kim Jong-un ambaye alitangaza kuteketeza vinu na eneo la
majaribio la silaha za maangamizi za kinyuklia za nchi hiyo.
Hata
hivyo, kuna mkanganyiko wa matakwa ya Marekani na inachofanya Korea
Kaskazini, ambayo imesema kuwa katika makubaliano yake na Korea Kusini,
walikubaliana kuharibu na kuachana na mpango wa silaha za nyuklia katika
eneo lote la Rasi ya Korea, kwa pande mbili.
0 comments:
Post a Comment