Mbunge
wa Bariadi (CCM), Andrew Chenge aliwahi kujiita nyoka wa makengeza
baada ya kutajwa katika mgawo wa Sh1.6bilioni zilizokuwa katika Akaunti
ya Tegata Escrow alizoingiziwa katika akaunti yake na mmoja wa wamiliki
wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, lakini jana Mei 10, 2018 amejibatiza
jina jipya la Bwana Reli.
“Mimi kuanzia leo mniite bwana reli. Niiteni jina langu hilo kuanzia leo. Kwa sababu nitakuwa nachangia kwa kila wizara hata kama sitahusika nayo.
“Mimi
nimshukuru Rais kwa uamuzi wake na tutaona tukapokamilisha reli hii,
uchumi wa Tanzania utaibuka kama uyoga, ikumbukeni tarehe ya leo, bwana
reli asema,” alisema Chenge jana Mei 10, jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Pamoja
na mambo mengine akichangia mjadala wa wizara hiyo Chenge alisema bado
anasumbuliwa na suala zima la gharama za uwekezaji nchini.
“Bado
zipo juu sana, naona kwenye hotuba hii hali ya upatikanaji wa umeme,
maji na miundombinu mingine yote bado inasuasua wakati inapaswa gharama
zishuke,” alisema.
Mwaka 2008, Chenge alipachikwa jina la ‘mzee wa vijisenti’ baada
ya kudaiwa kuwa na fedha ambazo zilikuwa ni zaidi ya Dola za Marekani
milioni 40 katika kashfa ya rada zilikuwa sawa na vijisenti.
Aidha,
mwaka 2009 Chenge alitawazwa kuwa mtemi wa kabila la Wasukuma-Bagole,
Kanda ya Itilima, wilayani Bariadi hivyo kupachikwa jina la ‘Mtemi Chenge’ .
0 comments:
Post a Comment